Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: marufuku wanafunzi kutozwa mchango kiholela


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ishirikiane na Sekretarieti  za  Mikoa na  Halmashauri zote kufuatilia matumizi na upatikanaji wa taarifa za fedha za Elimumsingi bila ada na zihakikishe wanafunzi hawatozwi  michango kiholela.

Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka taasisi hizo zihakikishe kuanzia sasa maelezo ya kujiunga na shule za umma (Joining Instructions) yanahakikiwa na kupewa idhini na Katibu Tawala wa Mkoa husika kwa kushirikiana na Maafisa Elimu wa maeneo husika.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 30, 2022) wakati akitoa Hoja ya Kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni jijini Dodoma. Amesema asilimia 10 ya fedha hiyo pia hutumika kugharamia huduma za umeme, maji na ulinzi.

“Pamoja na utekelezaji wa mpango huu, waheshimiwa wabunge wamelalamikia kuwepo utitiri wa michango shuleni. Aidha, Serikali kupitia waraka wa elimu namba tano wa mwaka 2015 na waraka wa elimu namba sita wa mwaka 2015 imetoa maelekezo bayana kuhusu utekelezaji wa Elimumsingi Bila Ada.”

Amesema maekezo hayo ni pamoja na matumizi ya fedha za utawala ambazo hutolewa HAZINA na kupelekwa moja kwa moja katika akaunti za shule za msingi na sekondari nchini kwa ajili ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ukarabati, uendeshaji wa mitihani  ya   ndani  na utawala.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono na dhamira yake kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kuhusu Serikali kutoa Elimumsingi Bila Ada kwa ngazi ya shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuimarisha mazingira ya utoaji wa elimu, mahudhurio na ufaulu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 yanaendelea vizuri na yamefikia asilimia 87, hivyo amewaomba wabunge hususan wanaporejea kwenye maeneo yao ya uwakilishi weendelee kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye zoezi hilo muhimu.

Vilevile, nitoe wito kwa Watanzania wote kujiandaa kuhesabiwa ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa sensa na viongozi kwenye maeneo wanayoishi. Zoezi hilo limepangwa kufanyika nchini kote Agosti 23, 2022.

Waziri Mkuu amesema zoezi hilo lilitanguliwa na Operesheni ya Anwani za Makazi ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 95 na Serikali imefanikiwa kukusanya taarifa na kutoa anwani za makazi zaidi ya milioni 12.

Sambamba na mafanikio hayo, Waziri Mkuu amezielekeza taasisi zote zenye dhamana ya masuala ya ardhi na makazi zihakikishe zinakuja na mikakati thabiti ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi iliyoainishwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi.

Waziri Mkuu amesema mbali na kuwa na mikakati ya kutatua migogoro ya ardhi, pia taasisi hizo pia zitoe miongozo ya namna bora ya kushughulikia changamoto za Watanzania kuishi katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na fursa zitokanazo na zoezi hilo.