Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Yonazi Atoa Wito kwa Watumishi Kujenga Tabia ya Kujifunza Ili Kuimarisha Uwajibikaji Serikalini


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, amewataka watumishi wa umma kujenga tabia ya kujifunza kwa bidii ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.

Dkt. Yonazi ametoa wito huo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa PEPMIS yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Ngome.

Akihimiza dhana ya kujifunza kwa kushiriki kikamilifu, Dkt. Yonazi alinukuu kauli maarufu ya Benjamin Franklin isemayo: “Niambie nisahau, nifundishe nitakumbuka, nishirikishe nijifunze.” 

Alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila mmoja akisema: “Tuchukue sehemu ya tatu ya kauli hiyo kwa sababu tunachohitaji ni kujihusisha ili tuweze kujifunza zaidi na kuimarisha utendaji wetu.”

Aidha, Dkt. Yonazi aliwataka watendaji wote kuchangamkia fursa hiyo ya mafunzo ya PEPMIS ili kupata maarifa mapya yatakayosaidia katika kutathmini na kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.

Kwa upande wake, Bw. Mutani Josephat Manyama – Mkufunzi wa Kitaifa wa Mfumo huo kutoka Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa umma kuhusu utekelezaji na tathmini ya utendaji kazi wao.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha viongozi na wasimamizi kufanya tathmini sahihi ya watendaji, jambo litakalosaidia maamuzi bora ya kiutumishi na kuongeza tija katika utumishi wa umma.