Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa awafariji waliopata ajali ya Precision Air


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Jumapili Novemba 6, 2022 amewasili Mkoani Kagera, na kushuhudia zoezi la uokoaji linaloendelea kufuatia ndege ya Precision Air kupata ajali ilipokuwa ikikaribia kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika eneo la ajali Waziri Mkuu amewasilisha salam za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakazi wa Bukoba na Tanzania kwa Ujumla.

“Rais Samia ameniagiza kuja kufuatilia zoezi hili na kuhakikisha linakwenda salama, pia ameguswa sana na tukio hili, na amekuwa akifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha zoezi la uokoaji linafanyika kwa mafanikio.”

Mheshimiwa Majaliwa amewashukuru wakazi wa Mkoa huo pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kujitokeza na kushiriki kutoa msaada na kufanikiwa kuwaokoa abiria 26.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa ukaribu zoezi la uokoaji pamoja na kusimamia kuitoa ndege hiyo katika eneo la ajali, na kutanabaisha kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Waziri Mkuu pia ametembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera na na kuwahakikishia kuwa watapewa huduma zinazostahili na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu huduma wanazopewa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mheshimiwa Waziri Mkuu majeruhi hao wameishukuru Serikali kwa kuwajari kwa kupatiwa huduma kwa haraka tangu walipookolewa kutoka katika eneo la ajali.

Mheshimiwa Majaliwa amesema mpaka sasa abiria 26 wameokolewa na kukiwa na miili 19 ambayo imetolewa katika eneo la ajali.