Habari
Katibu Mkuu Nzunda: Watumishi toeni Ushauri wenye weledi kwa viongozi wenu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Tixon Nzunda amewaasa watumishi wa ofisi yake kuendelea kutoa ushauri wenye weledi na kuzingatia taaluma katika kusaidia masuala ya Uratibu wa Shughuli za Serikali katika ofisi yake.
Kauli hiyo ameitoa mapema hii leo Aprili 9, 2021 wakati wa kikao cha kumuaga aliyekuwa katibu Mkuu wa ofisi hiyo (Sera na Uratibu) Bi. Dorothy Mwaluko katika ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo Mtaa wa Reli Dodoma.
Aliwaeleza kuwa viongozi wanatambua michango na ushauri wanaotoa kila wakati na kuhimiza waendelee kufanya hivyo bila kusita ili kuendeleza kasi ya utendaji katika ofisi yake.
“Ikumbukwe kuwa mshauri kazi yake si, kushauri mambo mazuri tu ambayo viongozi wangependa kuyasikia bali kutoa ushauri wenye weledi na kuzingatia taaluma na ifanyike hivyo hata kama wakuu hao wasingependa kusikia ukweli huo”
Kwa upande wake aliyekuwa katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bi. Dorothy mwaluko akizungumza na watumishi hao amewaasa watendaji wa ofisi hiyo kuendelea kuchapa kazi kwa ufanisi na kuendana na kazi ya Serikali yetu.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Bajeti wa ofisi hiyo Bw. Eleuter Kiwelle kwa niaba ya watumishi wa ofisi hiyo aliahidi kuenzi kwa vitendo yale mazuri waliojifunza kwa uongozi wa aliyekuwa katibu mkuu Bi. Mwaluku na kuahidi kuendelea kumuombea heri katika utuimishi wake wa umma.
“Kwa niaba ya watumishi wote, tunakushukuru kwa zawadi ya uwepo wako katika ofisi hii, na tunaahidi kuendeleza mazuri yote na kudumu katika nidhamu na weledi kiutendaji ili kuendeleza kasi ya maendeleo,”alisema Kiwelle.
“Tumejifunza mambo mengi kwako na kuonja upendo wako kwetu, hivyo tunaahidi kuendelea kuyaenzi katika utumishi wetu umma,”alisisitiza
=MWISHO=