Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi aipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Mji wa Serikali


Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Uratibu na Usimamizi mzuri wa Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Ametoa pongezi hizo mapema leo (05 Oktoba, 2023)alipokuwa katika ziara maalum ya Makatibu Wakuu ya kutembelea mji wa Serikali Mtumba Dodoma ambapo alisema mafanikio ya mradi huu wa ujenzi wa Mji wa Serikali ni kukamilika kwa ukamilifu wake akitolea mfano ujenzi wa Uwanja wa Mashujaa kuwa ni alama kubwa ambao utatumika kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na wageni kujifunza nini ambacho Tanzania imefanya.

“Tunathamini kazi yenu kubwa sana mnayofanya, kama tulivyosema awali kwenye Wasilisho, hii kazi inahitaji Uratibu kwa Sababu ni kazi ya Serikali, siyo kazi ya mmoja kuwa amemaliza na wengine kujisikia vibaya, tunashukuru kwa kutupitisha kwenye kazi kuanzia mwanzo, tumeona juhudi kubwa za wataalamu wetu na wasimamizi lakini pia tumeona kazi kubwa iliyopo mbele na tunatambua kwamba baadhi ya wadau wanakaribia kumaliza kazi zao.” Alisema Mhe. Balozi Kusiluka.

Aliendelea kusema kuwa bado kuna muda wa kutosha wa kutatua Changamoto ndogo zilizobainika katika ziara hiyo; na kusisitiza kuutazama mradi huo kwa ujumla wake kama Serikali moja, na kazi ya uratibu ikiendelea lakini pamoja na kuimarisha timu ya wataalamu wa ngazi zote katika ujenzi na kuwasikiliza, “Ni Fursa Pekee ambayo tumepewa ya kujenga Makao Makuu ya Serikali mapya  na Serikali imetoa fedha nyingi kwa hivyo ni lazima sisi wataalam tufanye kazi inavyopaswa.” Alisisitiza.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo, na kuwapa uhuru wataalam kufanya kazi ya kitaalam inavyopaswa, na kushauri wadau wengi kushiriki katika kazi hiyo pamoja na kujadili mambo ya kitaalam ili watu wengi waweze kujifunza.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema swala la ushirikishwaji wa wataalam katika ujenzi wa mji wa Serikali ni swala la muhimu sana, na wadau mbalimbali wanashirikishwa kwa ajili ya kuja kuwekeza katika maeneo mbali mbali  ambayo yametengwa katika mji huo wa Serikali,na majengo hayo ya Mji wa Serikali yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.

=MWISHO=