Habari
Dkt. Biteko ahimiza wanawake kutumia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wanawake nchini kutumia fursa ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa ajili ya kukopa na kujiongezea vipato.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo leo Septemba 14, 2024 mkoani Singida wakati akimwalilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwenye Kilele cha Maonesho ya Saba ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji kwa Mwaka 2024.
“Wanawake tumieni fursa iliyoweka na Serikali ya Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili muweze kukopa na kupata manufaa kutokana na mikopo hiyo. Natoa wito kwa benki zote nchini muwaaamini wanawake kwenye mikopo hii, mahali popote ukiona mwanamke anashughulika ujue faida inayopatika ni kwa familia yote,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amebainisha kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia alitoa wito kwa benki kuongeza kiwango cha kutoa mikopo kwa wananchi huku akitolea mfano Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambayo mwaka 2020 ilitoa shilingi bilioni 63 na hadi kufikia Agosti 2024 imetoa mikopo kiasi cha shilingi bilioni 337.
Ametaja takwimu za utoaji mikopo hiyo kutoka Benki ya TADB kuwa wanaume ni asilimia 58.1, vijana asilimia 19 na wanawake asilimia 22.4 huku akisisitiza benki nchini kuendelea kuongeza kiwango cha utoaji mikopo kwa wanawake.
“Mabenki endeleeni kuwaamini Watanzania, wakopesheni, punguzeni masharti lakini wenye uwezo wa kulipa wapeni mikopo ili waweze kufanyakazi.” Amesisitiza Dkt. Biteko.
Sambamba na hayo Dkt. Biteko amezindua Mwongozo wa Uratibu na Usimamizi wa Mifuko na Programu za Uwezeshaji ili iwe nyenzo ya kuimarisha utendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji kwa lengo la kuondoa changamoto zilizopo hasa mikopo chechefu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini katika jamii.
Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024. Amewaasa wananchi wa Singida na Watanzania kuchagua viongozi kwa kuzingatia sifa zao na si dini, fedha wala ukabila.
“ Ushiriki wenu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utawezesha kupata Viongozi wa Serikali za Mitaa ambao watachochea shughuli za uchumi na kusimamia vyema miradi pamoja na mifuko na programu za uwezeshaji zitakazokuwa zinaletwa katika maeneo yenu.” Amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Programu ya Uwezeshaji na elimu iliyotolewa mkoani Singida imegusa akina mama wengi na uwezeshaji huo utabadilisha maisha ya wananchi wa mkoa huo.
“ Programu za skimu za umwagiliaji zinalenga kupunguza umaskini kwa mtu mmoja mmoja na uwezeshaji wananchi kiuchumi umeleta mabadiliko makubwa mkoani kwetu,” amesema Dkt. Nchemba.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bi. Ben’g Issa amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwa na sera za kuwezesha wafanyabiashara wadogo.
Ambapo imeanzisha mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi na kutoa ruzuku katika sekta mbalimbali kwa kuwa bado wafanyabiashara wadogo hawapati mikopo kwa urahisi.
“ Serikali imekuwa ikifanya maonesho ya mifuko na programu za uwezeshaji ili kujenga uelewa kwa wananchi na kuonesha mifuko hii inavyoweza kubadilisha maisha yao, pia imeendelea na vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika mikoa yote Tanzania Bara ili kuhakikisha huduma mbalimbali ikiwemo mikopo, uongezaji thamani mazao, elimu ya kodi inawafikia wananchi.” Amesema Bi. Issa.
Aidha amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuimarisha programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia nchini inayolenga kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa za kushiriki katika shughuli za uchumi na kukuza vipato vyao.
Maonesho ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji hayo yameongozwa kwa kaulimbiu inayosema “Shiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Unufaike na Fursa za Uwezeshaji".
=MWISHO=