Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Simbachawene; tuenzi mambo mema yalioachwa na Mrema


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene ameomba wananchi kuenzi mambo mema yaliyoachwa kama alama wakati wa uhai wa Mhe.  Augustino Lyatonga Mrema.

“Tunamkumbuka kwa uzalendo wake wa kupenda demokrasia, lakini pia kupenda amani na utulivu katika itikadi zote. Mrema ni mtu mwenye rekodi kubwa katika siasa za ushindani wa nchi yetu”

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akitoa salamu za serikali katika ibada ya mazishi ya hayati Augustino Lyatonga Mrema iliyofanyika Marangu – Vunjo Mkoani Kilimanjaro.

"Sisi kama serikali tunaungana nanyi katika wakati huu mgumu; kushiriki msiba kwa moyo mkuu maana sisi sote  tunakwenda safari hiyo, yeye ametangulia sisi tupo nyuma yake, alisema waziri."

Ameeleza serikali na viongozi wakuu wanawapa pole Mama Watoto wa Marehemu na Wanakiraracha kwa ujumla na kipekee sana wanachama wote  wa TLP, chama ambacho amefariki akiwa ni Mwenyekiti wake wa  Kitaifa.

“ Marehemu Mrema amefariki akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole,na amefanya kazi yake vizuri alisema Waziri”

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Mhasham Baba Askofu Ludovick Minde, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Padre Deogratius Matiika wakili wa Askofu Jimbo Katoliki Moshi ametoa pole kwa wanafamilia na wale wote walioguswa na msiba.

Sisi kazi yetu kubwa ni kuendelea kumuombea ili Mwenyezi Mungu ampe furaha mbinguni, ameshiriki na sisi katika maendeleo ya jimbo letu, na tunashukuru Mungu kwa hayo aliyoyafanya.

“Nawaomba wanafamilia Mshikamane baba ameondoka msije mkagombana, mkae kwa amani na upendo, alisema Padre Matiika”