Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Simbachawene ashiriki maziko ya Padre Onesmo Wissi


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene ameshiriki ibada ya mazishi ya Padre Onesmo Wissi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dodoma, na baadaye mwili wake kuzikwa katika makaburi ya mapadre yaliyopo Bihawana Jijini Dodoma tarehe 28 Julai, 2022.

Akitoa salamu za Serikali, Waziri aliwaasa waumini na wanajamii wote kuyaenzi kwa vitendo mambo mazuri aliyoyafanya padre Wissi wakati wa uhai wake ikiwemo la utunzaji wa mazingira na ukarimu wake kwa watu wote bila kubagua.

“Padre Wissi alikuwa mtu wa watu mwenye kujali na kuhusika kwa ukaribu na wepesi popote alipohitajika, hakika tutamkumbuka kwa moyo wake wa upendo na ukarimu,” alisema Waziri

Padre Onesmo Wissi (62) ambaye wakati wa uhai wake alikuwa Makamu wa Askofu Jimbo Kuu Katoliki Dodoma nchini alifariki dunia katika Hospitali ya DCMC iliyopo Ntyuka mkoani humo alipopelekwa baada ya kujisikia vibaya.

Awali Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padre Paul Muhindi alisema kuwa, Padre Wissi alipelekwa katika hospitali hiyo Julai 25,2022 saa 1.00 jioni.

“Alianza kujisikia vibaya,akasema mbona hali inazidi kuwa mbaya akatupigia simu, tukaja na kum-rush (kumkimbiza) kule Ntyuka,” amesema Padre Muhindi.

Alisema Padre Wissi ambaye pia alikuwa Paroko wa Parokia ya Kanisa Kuu la Paul wa Msalaba, alifariki saa 3.00 usiku Julai 25, 2022 kwa ugonjwa wa kiharusi.

Misa ya mazishi ilianza saa 3.30 asubuhi katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Paul wa Msalaba na baadae kwenda kuupumzisha mwili wa marehemu katika makaburi ya mapadre yaliyopo Bihawana Jijini Dodoma.

=MWISHO=