Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu azindua mradi wa maji wilayani Mbulu


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi katika maeneo yote nchini vikiwemo na vijiji vya wilaya ya Mbulu.

Amesema kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ambayo ilianzishwa na Mheshimiwa Rais Samia akiwa Makamu wa Rais inamaanisha kumuwezesha wananchi kupata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi, hivyo amewasisitiza walinde vyanzo vya maji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Januari 24, 2022) baada ya kuzindua mradi wa maji wa Maghang-Maghang Juu-Gidimadoy wilayani Mbulu akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani Manyara.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti yenye lengo la kumaliza tatizo la maji nchini, hivyo wananchi waendelee kuiamini kwani kukamilika kwa mradi huo kumewawezesha wapate huduma hiyo ya maji safi na salama kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Awesu amesema Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya maji mkoani Manyara, ambapo ameahidi kuwa atahakikisha fedha hizo zinatumika katika utekelezaji wa miradi husika.

“Sisi Wizara ya Maji tutahakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao na kwamba hatutacheka na Mhandisi wala Mkandarasi anayejenga mradi wa maji kwani fedha ya Mheshimiwa Rais Samia haichezewi atakayethubu kuichezea jela inamuita.”

Awali, Meneja wa RUWASA wa wilaya ya Mbulu, Mhandisi Onesmo Mwakasege alisema mradi huo umewaondolea wakazi wa vijiji hivyo changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwani awali walikuwa wanapata maji kutoka katika visima vya asili.

Alisema chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu ambacho kina uwezo wa kuzalisha lita 43,000 kwa saa. “Ujenzi wa mradi huu uliotekelezwa kwa kutumia utaratibu wa force account na wataalam wa RUWASA ulianza Julai 1, 2020 na ulianza kutoa huduma Aprili 4, 2021.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mkazi wa kijiji cha Maghang Juu, Paulina Petro amesema wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwaondolewa adha ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma ya maji.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia, hii kwetu ni historia miaka yote hatujawahi kuona maji yakitoka katika kijiji chetu, maji tulikuwa tunayafuata kijiji cha jirani, tumeteseka kwa muda mrefu lakini sasa huduma hii ipo katika eneo letu.”

-END-