Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu azindua jengo la huduma za macho hospitali ya Bugando


 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua jengo la Idara ya Macho katika Hospitali ya Kanda  Bugando ambalo limekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa kwa kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za kibingwa za macho.

“Ujenzi wa mradi huu unakwenda kupunguza usumbufu kwa wagonjwa waliokuwa wakisafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 1,000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda hospitali ya KCMC au Muhimbili kwa ajili ya kupata huduma bora za macho.”

Waziri Mkuu amezindua jengo hilo leo (Jumapili, Oktoba 16, 2022) katika Hospitali ya Kanda  Bugando j[j[ni Mwanza akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu kukagua shughuli za maendeleo zinazotekeleza na Serikali mkoani hapa. Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 3.7.

Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi huo unaolenga Kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma bora za kibingwa na zinazokidhi matakwa na matarajio ya wagonjwa, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini likiwemo Kanisa Katoliki katika kuboresha huduma za jamii yakiwemo matibabu.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha utoaji wa huduma za jamii nchini imepanuwa wigo kwa kushirikisha sekta binafsi, taasisi za dini na mashirika mbalimbali. Kanisa Katoliki ni mojawapo ya taasisi ambazo serikali imeendelea kushirikiana nazo katika utoaji wa huduma za jamii.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema katika Hospitali ya Bugando Serikali imekuwa na ubia na kanisa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kugharamia mishahara kwa watumishi 1,191 sawa na asilimia 66 ya watumishi wote wa hospitali ambapo kila mwezi jumla ya shilingi bilioni 1.7 hulipwa na Serikali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Bugando, Dkt. Fabian Massaga amesema hospitali hiyo inatoa huduma kwa kushirikiana na Serikali na kwamba mradi huo uliozinduliwa leo unalenga kupunguza upofu unaozuilika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ujenzi wa mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100 ulianza Februali 3, 2021 na ulikamilika Juni 23, 2022.

Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia  Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya.

Naye, Askofu wa Jimbo Kuu la MwanzaMuhashamu Baba Askofu Mkuu Renatus Nkwande, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa ambao umewezesha hospitali hiyo kuongeza idadi ya madaktari wa macho. 

Muhashamu Baba Askofu Mkuu Nkwande amesema ongezeko hilo la madaktari limesaidia kuboresha huduma za tiba ya macho katika Kanda ya Ziwa. “Tangu kuanzishwa hospitali hiyo kwa  zaidi ya miaka 40 ilikuwa na daktari mmoja tu wa macho aliyehudumia kanda nzima lakini sasa tunao sita.”