Habari
Waziri Mkuu atoa rai kwa uongozi wa Chuo cha Ulinzi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa chuo cha Ulinzi cha Taifa uweke malengo endelevu yatakayokifanya kiwe kituo bora, bobezi, mahiri na chenye kutegemewa na Taifa katika masuala ya Ulinzi, usalama na mikakati.
Ametoa Wito huo leo Alhamisi (Julai 22, 2021) katika mahafali ya tisa ya Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC), katika kozi ya usalama na mikakati, kilichopo Kunduchi mkoani Dar Es Salaam.
Amesema Serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa chuo hicho Kinakuwa ni Kituo cha ufahari katika kutoa elimu ya juu kwa maafisa, watendaji kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na watumishi wa umma.
Ameongeza kuwa anatambua na kuthamini mchango wa chuo hicho katika kutoa mafunzo yanayowajengea uwezo viongozi na watendaji mbalimbali kwenye masuala ya usalama na mikakati.
“Hadi sasa maafisa waandamizi 300 kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ndani na nje ya nchi na wengine kutoka katika taasisi za umma za kiraia wamenufaika na programu hii inayotolewa na chuo cha Taifa cha Ulinzi”
Amesema kuwa chuo hiko kimeendelea kuwa sehemu muhimu katika kujenga na kuimarisha mahusiano ya mtu mmoja mmoja kwa washiriki wa program zake sanjari na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Waziri Mkuu pia amekitaka chuo hicho kihakikishe kuwa kinatoa mafunzo na utaalamu ambao utasaidia katika kukabiliana na matishio ya kiusalama ya karne ya 21 vikiwamo vitendo vya kigaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, dawa za kulevya, uhalifu wa kimtandao na janga la UVIKO-19.
Aidha, Waziri Mkuu amezishukuru nchi washiriki kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho na amewahimiza waendelee kuwaleta maafisa wao waandamizi kupata mafunzo kupitia chuo hicho.
“Nimefarijika kuwaona baadhi ya wahitimu wa programu hii kutoka nchi rafiki za Bangladesh, Burundi, Kenya, Nigeria, Malawi, Uganda na Zambia. Uwepo wenu ni kielelezo tosha cha imani mliyonayo kwetu hususani katika kuhakikisha viwango vya ubora vya chuo hiki vinasimamiwa ipasavyo”
Waziri Mkuu amewataka wahitimu hao kwenda kudhihirisha kile walichojifunza katika masuala ya ulinzi, usalama na mikakati. “Ninayo imani kuwa mmepata elimu ya kutosha kuwawezesha kushughulikia changamoto za kiusalama katika medani za sasa za kimataifa”
Pia, Waziri Mkuu amekitaka chuo hicho kuhakikisha kinafuatilia nyendo za wahitimu wake baada ya kumaliza masomo ili kuona matokeo ya kile walichojifunza.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Balozi Dkt. Marten Lumbanga amesema kuwa wataendelea kusimamia ubora wa masomo yanayotolewa chuoni hapo ili kukifanya chuo hicho kuwa na hadhi ya kimataifa katika utoaji wa elimu bora.
Wahitimu katika kozi ya Usalama na mikakati ni 40. Wahitimu wa Shahada ya Umahiri ni 28, Stashada 11 na Astashahada 1.
-End-