Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu atoa onyo kwa watoa leseni za uchimbaji


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa onyo kwa maafisa wanaohusika na utoaji wa leseni za madini kuacha tabia ya kuwazunguka wananchi wanaokwenda katika ofisi zao kuomba leseni za uchimbaji baada ya kubaini uwepo wa madini kwenye baadhi ya maeneo na kisha kuwapa wachimbaji wengine.

…Acheni tabia ya kuwaonea wananchi wanaotoka kwenye maeneo yenye fursa ya madini anakuja kuomba leseni ya kumiliki eneo hilo na unamwambia aache taarifa zake aje kesho kuchukua majibu akija kesho unamwambia eneo hilo limeshachukuliwa na mtu mwingine kumbe wewe unamtafuta mtu wa kuweza kumiliki ili upate chochote kitu, tukikugundua hatua kali zitachukuliwa dhidi yako. 

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Agosti 26, 2023) wakati akifunga Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji mkoani Lindi yaliyofanyika kwenye viwanja vya soko la Kilimahewa wilayani Ruangwa. Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania ufanye tafiti za madini za kimkakati kwa kushirikiana na halmashauri kwa lengo la kuwasaidia Watanzania kufanya shughuli zao kwa tija na kuhakikisha mipango sahihi ya matumizi ya ardhi inafikiwa.

Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zenye maeneo ya migodi ziweke mpango madhubuti wa kuhakikisha uchimbaji endelevu unaozingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira sambamba na kutoa elimu kwa umma kuhusu namna nzuri ya utunzaji wa mazingira hayo.

”Halmashauri zote zihakikishe zinatoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji waliobaini fursa ndani ya  maeneo yao. Uandaliwe mkakati rahisi na endelevu wa kuwezesha upatikanaji wa taarifa za fursa mbalimbali zilizopatikana kupitia maonesho haya."

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wachimbaji wote wa madini waweke kipaumbele katika kuyaongezea thamani madini hayo na kuzitumia taasisi za madini ili kufanya shughuli zao kwa tija, uhakika na faida zaidi.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake mazuri ya kutengeneza mazingira ya kuvutia wawekezaji. ”Ndugu zangu tusijidanganye hakuna maendeleo bila ya uwekezaji.”

Amesema uwekezaji unatoa fursa mbalimbali zinazochangia katika kuchochea maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla kwa kutoa ajira nyingi, hivyo aliwasisitiza wana-Lindi waendelee kutoa ushirikiano kwa wawekezaji.

Pia, Mheshimiwa Kikwete ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Lindi waendelee kulinda rasilimali mbalimbali ikiwemo ardhi. ”Zindukeni, jitahidini kuhifadhi rasilimali zenu, tumieni fursa ya kuwekeza au kuingia ubia na wawekezaji. Utauza ekari moja kwa shilingi laki moja leo baada ya miaka mitano mtu anaiuza kwa shilingi milioni 100.”