Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu atoa agizo kwa RPC Lindi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi ahakikishe wafugaji wote walioingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kusababisha uharibifu wa mazao na wananchi kukosa chakula wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwani hakuna yeyote aliye juu ya sheria wananchi wote ni sawa.

“Serikali iko macho na itamchukulia hatua yeyote anayeathiri shughuli za wengine, Tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, hivyo watendaji wote wa vijiji wawajibike kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuepusha migogoro isiyokuwa na tija. Tutaendelea kuwalinda wananchi. Ukifuata utaratibu hakuna shida, tufuate sheria.”

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Novemba 15, 2023) wakati akizungumza na wananchi kwenye vijiji vya Namkatila, Matambarale na Nandandala akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Vijiji hivyo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo mkulima mmoja aliuawa.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa Serikali haitovumilia kuona jamii ya wafugaji wasiozingatia sheria na haitotoa nafasi kwa wakulima kuendelea kuharibiwa mazao yao. “Jambo hili halikubaliki na hatua kali zitachukuliwa kwa watu wote wanaotaka kuvuruga amani, Serikali haitovumilia vitendo hivyo.”

“…Hatutamsamehe mfugaji anayetumia fimbo yake kumpiga mkulima baada ya kulisha mifugo kwenye shamba lake. Hatuna nafasi ya kushuhudia hayo, utaratibu lazima uzingatiwe, lazima tukomeshe migogoro ya wafugaji na wakulima. Tumuache mkulima aendelee kulima avune. Tusilinde waovu.”

Waziri Mkuu amesema kwamba kauli ya Serikali ya kuthamini shughuli za kilimo na ufugaji nchini haimaanishi kuwa wafugaji wanaruhusiwa kuingiza mifugo na kulisha kwenye mashamba ya wakulima, wala wakulima kudhuru mifugo ya wafugaji hivyo amewasisitiza wafanye shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu kwani tayari serikali imeshaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya makazi, huduma za kijamii, kilimo na mifugo hivyo hakuna mwenye haki ya kumvamia mwingine.

Amesema watendaji wa vijiji wahakikishe kabla ya kuwakaribisha wafugaji katika maeneo yao wajiridhishe kama wana maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli hiyo na pia wawashirikishe wanakijiji husika juu ya ujio wa wafugaji na wafahamu idadi ya mifugo waliyonayo. “Wananchi tulieni mkiona maeneo yenu yamevamiwa toeni taarifa. Hapa tusisikie tena athari hizi.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi hao waendelee na shughuli zao za kilimo na wasiogopewa kwani Serikali ipo makini na inaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini vikiwemo na vijiji vyao. Wananchi hao walimuelezwa kuwa wanaogopa kuendelea na maandalizi ya mashamba kutokana na kuhofia uvamizi wa mifugo.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa wananchi lazima wafikishiwe huduma mbalimbali za kijamii karibu na makazi yao, hivyo kwa kushirikiana na watendaji wengine wa Serikali atahakikisha miradi yote ya maendeleo inasimiwa na kutekelezwa ipasavyo ikiwemo kukamilika kwa wakati na kwa viwango kusudiwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya wananchi wa kijiji cha Namilema kumuomba awasaidie kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi ambao wamekamilisha ujenzi wa boma. Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya ahakikishe zahanati hiyo inakamilika.