Habari
Waziri Mkuu atoa agizo kwa MSD
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wiki mbili kwa Bohari ya Dawa (MSD) ihakikishe kuanzia leo Januari 23, 2022 hadi ifikapo Februari 5, 2022 iwe imeshafikisha vifaa vyote vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Manyara kwa kuwa tayari fedha zimeshalipwa.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maagizo kuwa vituo vyote vya afya vinapokamilika vianze kutoa huduma, hivyo MSD lazima ihakikishe inafikisha vifaa katika vituo hivyo haraka. Majengo ya kutolea huduma yameshakamilika tunataka tuone yakitumika na yasipotumika yataharibika."
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Januari 23, 2022) alipokagua mradi ya ujenzi wa kituo cha afya cha Mogitu kilichopo wilayani Hanang’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani Manyara
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya nchini, hivyo kukamilika kwa kituo hicho cha afya cha Mogitu kunalenga kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu wa kufuata huduma hizo katika kituo cha afya cha Kata ya Katesh.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Hanang Dkt. Boniface Manditi ahakikishe kituo hicho kianzaa kutoa huduma za afya kwa wananchi kwa kuwa tayari ujenzi wake umekamilika.
Naye, Mganga Mkuu wa wilaya ya Hanang’ Dkt. Manditi amesema gharama za utekelezaji wa mradi huo ni sh. milioni 578,926,000 ambapo kati yake sh. milioni 400 zimetolewa na Serikali Kuu, sh. milioni 125,726,000 zimetolewa na Halmashauri ya Hanang’ na mchango wa wananchi ni sh. milioni 53,200,000. Dkt. Manditi amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa kuanzia kesho Jumatatu Januari 24, 2022 huduma zitaanza kutolewa kituoni hapo.
Amesema kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia jumla ya wakazi 11,725 kutoka katika vijiji vitatu vya kata ya Mogitu ambavyo ni Mogitu, Gabadaw, Gidagamowd na wakati wa maeneo ya jirani. Amesema mradi huo uko katika hatua za ukamilishaji ukiwemo ukamilishaji wa mifumo ya maji safi na maji taka.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amerejea kauli ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa jana wakati akizindua tamasha la utamaduni wa Kilimanjaro ya kuwataka wananchi wakakikishe wana tunza chakula walichonacho na watumie mvua zilizoanza kunyesha kwa kupanda mazao ya muda mfupi.
Waziri Mkuu amesema kwa kuwa msimu wa mvua umechelewa wananchi watumie mvua zilizoanza kunyesha kwa kupanda mazao ya muda mfupi. “Tujitahidi kuhifadhi chakula tulichokuwa nacho na tujiepushe na shughuli za kijamii zinazotumia chakula kingi ili tuwe na akiba ya chakula ya kutosha na wanaouza chakula wauze kwa utaratibu mzuri.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji wa Mogitu-Katesh uliogharimu sh. bilioni 2.4. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha lita milioni 2.5 kwa siku huku mahitaji ya wakazi wa maeneo hayo ni lita milioni 2.4 kwa siku.
Amesema utekelezaji wa miradi ya maji nchini ni mkakati maalumu wa Mheshimiwa Rais Samia wa kumtua mama ndoo kichwani ambao aliuanza tangu akiwa Makamu wa Rais, hivyo amewata viongozi wanaotekeleza miradi hiyo wahakikishe malengo yanafikiwa na wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao.
-END-