Habari
Waziri Mkuu ataka uwiano sawa wa walimu kati ya mijini na vijijini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Elimu na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wafanye mapitio ya ikama zao kuangalia mlundikano wa walimu katika maeneo ya mijini na pembezoni mwa barabara na kuwasambaza katika maeneo ya vijijini ili kuwe na utoshelevu wa walimu katika maeneo yao.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 16, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Keneth Nollo katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni, Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuruhusu Majiji na Halmashauri zenye uwezo waweze kuajili walimu na kuondoa tatizo la upungufu wa walimu.
Waziri Mkuu amesema Serikali imesimamia mifumo ya ajira na ajira zote za kudumu ziko chini ya Serikali Kuu ikiwemo na za sekta ya elimu kwa walimu, upungufu huo licha ya mambo mengine pia unachangiwa na mpango usiokuwa mzuri wa kusambaza walimu kwenye baadhi ya halmashauri. “Walimu wengi wanaonekana mijini kuliko vijijini.”
“Lengo la kuwa na mfumo mmoja wa kuajiri na kupata kanzidata ya idadi ya waliopo kazini, wanaoajiriwa lakini pia kusambaza kwa usawa kwenye halmashauri zote ili kusiwe na halmashauri moja kuwa na mlundikano mkubwa kwa sababu tu wana uwezo wao kuajiri kwa hiyo. Serikali Kuu inasimamia kusambaza walimu kulingana na mahitaji.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Tanzania ina sheria za kazi ambazo zinaainisha muda wa kuingia na kutoka kazini na kwa mujibu wa sheria hizo muda wa kazi kiserikali ni masaa manane kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi 9.30 alasili.
Ameyasema wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mariam Kisangi ambaye alitaka kufahamu Serikali imejipange katika kupitia upya utaratibu wa watumishi wa kada moja kutoka kazini. Alisema walimu wa mijini na vijijini wamekuwa wakitofautiana muda wa kutoka kazini.
Waziri Mkuu amesema utofauti wa muda wa kutoka kwa walimu wa vijijini na mijini ni mazingira ya maeneo hayo kwani maeneo ya mijini wanafunzi na walimu wakiingia asubuhi, mchana hawapati muda wa kupumzika hivyo huunganisha hadi saa 9.30 na vijijini hupata muda wa nafasi ya kwenda kula na kurudi tena na muda huo ndio unaofidiwa, masaa ya kazi ni yale yale.
“Huu ni mpangokazi uliowekwa kulingana na mazingira yaliyopo, kwa nini mjini waamua kuunganisha moja kwa moja, kwanza kuna shida ya usafiri huwezi kumruhusu mchana arudi nyumbani na aende tena shule ni shida lakini vijijini kwa kuwa hakuna tatizo la usafiri wanatembea kwenda na kurudi ”.