Habari
Waziri Mkuu amwakilisha Rais Samia mkutano wa Vijana wa Dunia
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Jukwaa la Nne la Vijana Duniani lililoanza leo jijini Sharm-El-Sheikh, Misri.
Akishiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao leo mchana (Jumatatu, Januari 10, 2022) kutoka ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Waziri Mkuu ameyaomba mataifa makubwa duniani yashirikiane na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ili kuhakikisha uchumi wa nchi hizo unarejea katika hali yake ya kawaida kutokana na madhara ya UVIKO-19.
“Tangu kuingia kwa wimbi la kwanza la UVIKO-19, tumeshuhudia athari kubwa za kiuchumi na hasa kwa vijana. Vijana wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu lakini uwepo wa UVIKO-19 umeathiri maendeleo ya sekta ya utalii ambapo vijana wengi wameajiriwa.”
Ameongeza kuwa UVIKO-19 umeathiri uwekezaji katika viwanda na kwenye sekta ya miundombinu ambako makampuni mengi yalitoa ajira kwa vijana lakini hayakuweza kufanya kazi na hivyo kuleta athari kubwa.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia alipata fursa ya kuzungumza katika mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Marekani mwaka jana ambako alieleza athari za ugonjwa wa UVIKO-19 na Tanzania ikaweza kupata mkopo nafuu uliotumika kujenga madarasa na vituo vya afya kama njia ya kurejesha uchumi.
“Tumehamasisha Umoja wa Afrika (AU) ulichukue suala hili kama ajenda ili uweze kujadili namna bora ya kurejesha uchumi wa Afrika; Tanzania ikiwa mwanachama wa AU nayo pia itaingia kwenye mjadala huu na tutapata njia bora ya kurejesha uchumi wetu hasa tunapolikabili wimbi la nne.”
Amesema Tanzania imeonesha inahitaji kuungwa mkono katika jitihada zinazochukuliwa kwenye ujenzi wa miundombinu ili Watanzania na hasa vijana waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa jumla wa kitaifa.
Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni Rais wa Misri, Bw. Abdel Fattah Al-Sisi, Rais wa Colombia, Bw. Ivan Derque Marques, Rais wa Romania, Bw. Klaus Iohannis, Rais wa Zambia, Bw. Hakainde Hichilema, Rais wa Malta, Bw. Malta George Vella na Waziri wa Nchi wa Falme za Kiarabu anayeshughulikia Masuala ya Vijana, Bi. Shamma al Mazrui.
Mkutano huo wa siku nne ambao unashirikisha wajumbe zaidi ya 5,000 kutoka nchi mbalimbali duniani, unalenga kujadili madhara ya UVIKO-19 kwa vijana na namna gani nchi zimeweka mikakati ya kukabiliana nazo katika shughuli za kiuchumi, mabadiliko ya tabia nchi, hifadhi za jamii, haki za binadamu na uhifadhi wa mazingira.
(mwisho)