Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu akaribisha wawekezaji kutoka China


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia sasa China imewekeza zaidi ya dola bilioni 10 katika maeneo mbalimbali nchini na ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine zaidi.

Amesema kuwa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa  kuna zaidi ya miradi 1,134 ambayo imesajiliwa kutoka makampuni ya China na hivyo kuchangia ajira kwa Watanzania.

Ameyasema hayo leo jioni (Jumatatu, Septemba 25, 2023) wakati akifunga Kongamano la Uwekezaji na Biashara baina ya Tanzania na China kwa udhamini wa Jimbo la Zhejiang (Jinhua) kwenye  hoteli ya Rotan jijini Dar es Salaam.

“Miaka 10 iliyopita, China ilikuwa nchi ya sita miongoni wa wawekezaji wakubwa hapa nchini ikitanguliwa na Uingereza, Marekani, Afrika Kusini na Kenya. Lakini kutokana uwekezaji wa sasa, imekuwa nchi ya kwanza kwa uwekezaji hapa nchini,” amesema.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora na rafiki ya uwekezaji ikiwemo kufanya maboresho ya sera ya uwekezaji. “Tumewahakikishia kuwa tumefanya maboresho kwa kuondoa urasimu, mlolongo wa vikwazo kwa kuweka one stop centre kwenye kituo chetu cha uwekezaji.”

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekeze Dodoma ambako ni makao makuu ya nchi hasa kwenye maeneo ya ujenzi wa makazi na ofisi.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi (OR- Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo alisema kongamano hilo limehudhuriwa na wafanyabiashara 300 wakiwemo 200 kutoka Tanzania na 100 kutoka China.

Amesema kuandaliwa kwa kongamano hilo ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza suala la kuvutia wawekezaji nchini.

Naye Balozi wa China hapa nchini, Bi. Chen Mingjian alisema tangu kumalizika kwa ugonjwa wa UVIKO-19, uwakilishi wa makundi nane ya wafanyabiashara kutoka miji na majimbo ya China yamekwishatembelea Tanzania ili kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji.

“Kutokana na uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka China, bidhaa za saruji, chuma, ceramics, vifaa vya ujenzi na bidhaa za urembo na sabuni zimezalishwa nchini na kutoa ajira zaidi ya 150,000,” alisema.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema wafanysbiashara wa China wanakaribishwa kuwekeza katika sekta mbalimbali hasa kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na bidhaa nyingine zinazozalishwa nchini.

“Tunaamini tukiwa na viwanda hivyo, tutaongeza ajira kwa vijana wetu lakini pia tutaweza kuuza nje ya nchi bidhaa zilizoboreshwa badala ya kuuza mali ghafi.”