Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu aagiza stendi kuu Bariadi itumike kwa mabasi makubwa na madogo


 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza stendi kuu ya mabasi katika mji wa Bariadi mkoani Simiyu ianze kutumika kwa mabasi makubwa na madogo ili kuondoa usumbufu kwa abiria.

"Mkuu wa Mkoa wekeni utaratibu utakaofaa ili mabasi yaanzie pale na kuishia pale lakini haimaanishi kuwa muwapitilize abiria wanaoshukia au kupandia njiani.”

Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Jumapili, Machi 26, 2023) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Mji wa Bariadi katika eneo la stendi ya zamani akiwa njiani kuelekea Maswa.

“Jana nilitembelea pale stendi kuu na kuona fedha za Serikali zinapotea bure. Kuna vibanda 148 vya wajasiriamali lakini hawafanyi kazi kwa sababu hakuna abiria wanaoingia na kutoka. Kuna vijana wa bajaj na bodaboda wamejipanga vizuri lakini hawana kazi kwa sababu hakuna mabasi,” amesema.

Amesema Serikali ilitoa sh. bilioni 7 ili zitumike kuupanga mji wa Bariadi na pia ikaanzisha mfumo wa anuani za makazi ili uwepo urahisi wa kufikika. “Lazima tujipange vizuri ili mji huu upangike. Huu mji ni makao makuu ya mkoa, kwa hiyo malori hayatakiwi kupaki holela hapa mjini bali yaende kwenye eneo lake lililotengwa.”

Akifafanua kuhusu eneo la kupaki malori, Waziri Mkuu amesema kuwepo kwa malori katika eneo hilo kutafungua ajira kwa vijana mafundi wa magari, mafundi umeme, wauza vipuri na mafundi gereji. “Wote waende kule na Halmashauri waboreshe lile eneo kwa kuweka huduma zote za msingi,” amesisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema viongozi wa mkoa huo hawapaswi kuwabana wajasiriamali bali wawaelimishe na kuwapa miongozo ili wajiendeleze kiuchumi.

Ametoa kauli hiyo kuhusiana na suala la biashara ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari madogo aina ya probox ambayo yalikuwa yamezuiliwa na uongozi wa mkoa huo. “Viongozi nimewaomba msiwabane vijana wajasiriamali, msiwazuie kujiendeleza kiuchumi, cha msingi wapeni miongozo, wapeni elimu. Na vijana ni lazima mzigatie usalama wa gari na abiria na kufuata sheria zilizowekwa,”

“Mkuu wa Mkoa ofisi yako ilisitisha matumizi ya magari haya maarufu kwa jina la mchomoko na sasa tumefungua milango. Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan alikwishaelekeza kuwa hawa wajasiamali wadogo wawezeshwe.”

Amewataka madereva wa magari hayo wafanye usajili LATRA na kwa maafisa Biashara na kuzingatia sheria zote za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kupakia abiria sawa na uwezo wa chombo hicho.

"Mkianza kusajili madereva, Jeshi la Polisi nendeni mkatoe elimu ili watu wafanye biashara kwa kufuata sheria. Tukiacha mambo yaende holela, tutajikuta tunatengeneza utamaduni ambao utawakwaza ninyi na wao pia watakwazika," amesema.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya Mkoa wa Simiyu kwa kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya ya Maswa.