Habari
Wasindikaji wa Vyakula watakiwa kuzingatia sheria ya Chakula.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama amewataka wamiliki wa viwanda vikubwa vya usindikaji wa chakula nchini (Unga wa ngano,Unga wa Mahindi na Mafuta ya kula) kuhakikisha wanaweka virutubishi katika bidhaa hizo kama inavyowataka Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2010.
Sheria hiyo chini ya kanuni zake inawataka wamiliki wa viwanda vikubwa vya usindikaji wa chakula nchini kuongeza virutubishi vya madini joto kwenye chumvi na kuongeza virutubishi vya madini ya chuma, zinki, Asidi ya foliki na Vitamini B 12 kwenye unga wa ngano na mahindi pamoja na virutubishi vya vitamin A kwenye mafuta ya kula.
Waziri Mhagama ametoa agizo hilo jijini Dar es salaam wakati wa ziara ya kujionea hali ya urutubishaji wa vyakula hivyo, katika viwanda vya 21st Century Food and Packaging, Lina Millers Ltd na Neelkanth Salt Ltd pamoja na kuangalia wigo wa urutubishaji wa vyakula katika kuwafikia walengwa.
Waziri Mhagama amesema kwenye urutubishaji wa unga wa mahindi bado viwanda vingi havifanyi vizuri kwani ni asilimia saba (7%) pekee ya unga unaozalishwa nchini ndiyo unaongezewa virutubishi hivyo hali inayosababisha watumiaji wengi wa unga kukosa Vitamini na Madini muhimu Mwilini.
“Tumeweka sheria na tayari tumeanza kuitumia toka mwaka 2013 kuhakikisha vyakula vinavyozalishwa nchini vinaongezwa virutubishi, hivyo ni jukumu la kila mwenye kiwanda kuzinzingatia sheria hii kwani vyakula hivi vitasaidia kupunguza tatizo la udumavu nchini, ambalo kwa kiasi kikubwa tumeweza kukabiliana nalo,” Amesema Waziri Mhagama
Amefafanua kuwa Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuandaa Sheria ya Chumvi ya Mwaka 1994. Sheria hiyo imefanyiwa mapitio na kuwa kanuni chini ya Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2010 ili kuhakikisha kuwa chumvi yote inayotumika nchini kwa ajili ya matumizi ya binadamu na wanyama inaongezewa madini joto.
Akizungumzia kiwango cha uongezaji virutubishi kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa nchini, Waziri Mhagama amesema kwa upande wa mafuta wamiliki wengi wa Viwanda hivyo wameonekana kuweka jitihada kwani mpaka sasa mafuta yanayozalishwa na viwanda vya ndani asilimia 73 yanaongezewa virutubishi.
“kuna faida nyingi sana katika urutubishaji wa unga na mafuta, bila shaka kila mmoja wetu anafahamu, vyakula hivi vitasaidia kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano, pamoja na vifo vya wanawake wajawazito.” Amesema Waziri Mhagama
Katika Hatua nyingine Waziri Mhagama pia aliutaka uongozi wa Kiwanda cha kuzalisha Chumvi cha Neelkhanth Salt kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani ambapo nao amewataka kuzingatia sheria ya Chumvi ya Mwaka 1994 kama ilivyofanyiwa mapitio na kuwa kanuni chini ya sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 201 inavyowataka wazalishaji wa chumvi kuhakikisha chumvi yote inavyozalishwa nchini inawekewa madini joto.
Aidha, Waziri Mhagama amezipongeza Taasisi zisizo za kiserikali, kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa Wamiliki wa viwanda vya usindikaji wa chakula (Unga wa ngano, unga mahindi na mafuta ya kula) wanakuwa mstari wa mbele katika zoezi la urutubishaji linafanyika ipasavyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu.
Nae Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha unga cha Lina Millers Ltd Lina Kimaro alisema bado jamii inahitaji elimu zaidi kuhusu vyakula vinavyoongezwa virutubishi, kwani changamoto ambayo wamekutana nayo kwa baadhi ya wateja wao ni kushindwa kukubali vyakula vilivyo ongezwa virutubishi.
Wakiongea kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, Meneja Mrad kutoka Technoserve Tanzania George Kaishozi pamoja na Meneja Mradi wa urutubishaji vyakula, Gain Tanzania, Archad Ngemela, wamebainisha kuwa watendelea kuunga mkono jitihada za serikali juu ya urutubishaji na uzalishaji bora wa chakula nchini.
Mwaka 2011 Viwango na kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula viliandaliwa, ambapo Mwaka 2013, Uongezaji virutubishi ulizinduliwa rasmi hapa nchini. Hadi sasa jumla ya viwanda vikubwa na vya kati 35 vya ngano, mahindi na mafuta ya kula vinaongeza virutubishi kwenye vyakula. Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 88 ya ngano na asilimia 68 ya mafuta yanayozalishwa na viwanda vikubwa vinaongezwa virutubiishi ipasavyo.