Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mhagama: Rais Samia atenga zaidi ya Tsh. Bilioni 600 Ujenzi Awamu ya Pili Majengo ya Serikali Mtumba


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema Rais wa Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametenga zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali awamu ya pili ili majengo hayo yaanze kutumika kwa haraka.

Ameyasema hayo hii leo Oktoba 18, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa majengo mapya ya Ofisi ya Waziri Mkuu awamu ya pili katika  Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama alisema kuwa, toka Serikali ilipotangaza azma ya kuhamishia shughuli zake Makao Makuu ya nchi, mwezi Septemba, 2016, hadi kufikia Juni, 2021 jumla ya Watumishi 18,300 wamekwisha hamia Jijini Dodoma na katika kipindi hicho shilingi bilioni 655, 886, 878, 308.83 zilitumika kuhamisha watumishi  pamoja na kuwezesha ujenzi wa majengo ya Ofisi za Awali za awamu ya kwanza na miundombinu muhimu katika Wizara 23.

“Nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza nia na maamuzi ya Serikali kuhamia Jijini Dodoma kwa vitendo pamoja na kuridhia mpango mkakati wa ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali awamu ya pili,” alisema Waziri Mhagam 

Alifafanua kuwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia jumla ya shilingi bilioni 600, 884, 941, 784.70 katika kuhakikisha awamu ya pili ya ujenzi wa mji wa Serikali yanakamilika.

 “Katika mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi bilioni 300 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo ya serikali,” alisema

 Aliongeza kuwa, ujenzi wa majengo katika mji wa Serikali awamu ya pili yatakuwa na muundo wa ghorofa na kila jengo litakuwa na ghorofa 6 kwenda juu na hapatakuwa na  jengo lenye idadi ndogo ya ghorofa hizo.

 “Kipekee Ofisi ya Waziri Mkuu tunampongeza Mhe. Rais kwa kupata fursa ya kujenga majengo mawili kupitia ujenzi huu wa majengo haya ya Serikali katika awamu hii ya pili,” alisema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa Wizara zote kukamilisha kwa haraka utaratibu wa kupata wakandarasi kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mikataba yote ya ujenzi ihakikishwe inazingatia thamani ya fedha na viwango katika ujenzi unaotarajiwa kuanza, Taasisi zinazohusika na huduma na miundombinu zihusishwe katika ujenzi na utekelezaji wa Mradi  Taasisi ikiwemo, DUWASA, TANESCO, TTCL, Zimamoto, NEMC, OSHA, TFS na GSO na pia amezitaka kamati za ndani za ufuatiliaji na usimamizi kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi na changamoto zinazojitokeza ili kuzipatia ufumbuzi.

Aidha, Waziri alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi wa jiji la Dodoma kuchangamikia fursa mbalimbali wakati wa ujenzi wa majengo hayo ya Serikali katika awamu hii ya pili.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Tixon Nzunda aliahidi kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Waziri huku akimuhakikishia kusimamia mradi huo kwa viwango vinavyo hitajika na kukabidhi mradi huo kwa wakati.

“Tumesha saini mkataba na kumaliza taratibu za manunuzi na kukabidhi rasmi kazi za ujenzi kuanza na hadi sasa kazi za awali zinaendelea ikiwemo kusafisha eneo la mradi. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 16 badala ya miezi 24 kama ilivyokuwa awali,” alisema Nzunda