Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mhagama awaasa watendaji Ofisi ya Waziri Mkuu kuendeleza uzalendo


Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu  wameaswa kuzingatia uzalendo na matumizi sahihi ya rasilimali zinazotolewa ikiwemo fedha  katika kutekeleza majukumu yao ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano .

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama leo Machi 12, 2021 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo ambapo amesema kuwa Ofisi hiyo ina dhima kubwa katika kuratibu shughuli za Serikali hivyo lazima watumishi na watendaji wote wakazingatia umuhimu wa Ofisi hiyo katika kutekeleza majukumu yao.

“Tunapotekekeleza majukumu yetu kwa uzalendo na weledi tunaonesha mfano bora kwa Wizara zote kama waratibu wa shughuli za Seriakali na pia tunamsaidia Mhe. Waziri Mkuu katika utekelezaji wa shughuli zote za kila siku za Serikali hivyo niwaase kufanya kazi kwa bidii zaidi”, alisema Mhe. Mhagama

Akifafanua, amesema kuwa Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamataja Mhe. Waziri Mkuu kuwa Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali hivyo ni vyema kila mjumbe wa  kikao cha baraza la wafanyakazi wa Ofisi hiyo akazingatia kuwa Ofisi ina majukumu  makubwa yakusimamia  na kuratibu shughuli za kila siku.

Aidha, Mhe. Mhagama amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo  kuhakikisha kuwa wanatatua kero za wafanyakazi  walio chini yao kwa wakati ili kuendelea kudumisha taswira nzuri ya Ofisi hiyo na pia kuwataka kuwa tayari kubadilika na kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kwa kuweka mpango bora wa mafunzo unaogusa watumishi wote.

“Watumishi wote oneni kuwa mnachangamoto ya kuendelea kuzingatia uzalendo na weledi katika kupiga vita rushwa na ufisadi ili kuendeleza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa manufaa ya wananchi wote”, alisisitiza Mhe. Mhagama

Pia, Mhe Mhagama alitoa wito kwa menejimenti ya Ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kazi nzuri iliyofanyika katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano iendelee kwa kasi zaidi na kwa wakuu wa Idara na vitengo kuendeleza ushirikiano na walio chini yao.

Akieleza zaidi amesema kuwa ushirikiano kati ya viongozi na watumishi unajenga upendo sehemu ya kazi na hiyo ni moja ya nyenzo muhimu katika kuleta ustawi wa watumishi na wananchi kwa ujumla kupitia huduma watakazopatiwa.

Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kimefanyika leo Jijini Dodoma ili kuwezesha kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/ 2021 na kupitia makadirio ya Mpango wa Bajeti wa Ofisi hiyo kwa mwaka wa Fedha 2021/ 2022.

=MWISHO=