Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

WAZIRI MHAGAMA ATOA AGIZO KWA KAMISHENI YA TUME YA UDHIBITI UKIMWI (TACAIDS)


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Kamisheni ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI, (TACAIDS) kusimamia ipasavyo mikakati ya kukabili mambukizi mapya ya virusi ya UKIMWI nchini.

Kauli hiyo ameitoa leo Agosti 10, 2021 jijini Dodoma wakati akizindua Kamisheni ya TACAIDS ambapo alitaja maeneo yanayohitaji jitihada ikiwemo Vijana ambao wanatajwa kuwa hatarini kupata maambukizi.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na kuhamasisha upimaji kwa wanaume na Watoto,kuimarisha huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,kuondoa ubaguzi na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU.

"Kuna maeneo mengine ambayo kamisheni inatakiwa kufuatilia kwa ukaribu kufuatilia matumizi ya rasilimali fedha na watu ndani ya tume na mfuko wa UKIMWI pamoja na mkakati wa usambazaji wa kinga na tathimini ya mkakati wa Dunia unaokwisha na ujao wa ndani," alisema Waziri Jenista.

Akizungumzia hali ya maambukizi nchini alieleza kwamba Takwimu zinaonyesha Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano ya VVU kwani kiwango cha upimaji wa afya kimeongezeka kutoka asilimia 61 kwa mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2019.

"Matumizi ya dawa za kufubaza VVU yameongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 Hadi asilimia 98 mwaka 2019, vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kutoka 64,000mwaka 2010 Hadi 32,000 mwaka 2020 na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yameshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020," alibainisha Waziri huyo.

Kwa upande wa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alihimiza ushirikishwaji wa kundi la watu wenye ulemavu katika kamisheni hiyo kurahisisha kufikisha mapendekezo na ushauri kulinda nakusimamia haki za watu wenye ulemavu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na ambao hawajapata maambukizi.

"Katika vita hivi hatuwezi kuliacha kundi la wenye ulemavu tunatambua wapo wanaoishi na maambukizi na wengine hawana hivyo uwepo wa mwakilishi angalau mmoja katika kamisheni hii itakuwa msaada mkubwa watafikiwa kwa urahisi," alifafanua Naibu Waziri huyo.

Katika hatua nyingine Naibu Katibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Kasper Mmuya anayeshughulikia alihimiza kuweka vyanzo vya fedha vya ndani ya Nchi ili kutoa huduma bora zitakazowesha kuendelea kulinda afya za wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya TACAIDS,Tanzania Dk. Hedwiga Swai alibainisha kwamba kufanikisha vita dhidi ya UKIMWI inahitaji ushirikiano wa taasisi zote, taasisi za dini na kila mmoja kwa nafasi yake kufikia malengo ya kimataifa ifikapo 2030 kutokomea maambukizi mapya n vifo vitokanavyo na UKIMWI na unyanyapaaji.