Habari
Waziri Mhagama aongoza Harambee ununuzi vifaa vya elimu na saidizi kwa Shule ya Libermann Viziwi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameongoza harambee maalumu ya ununuzi wa vifaa maalumu vya kielimu na saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya Libermann Viziwi.
Halfa hiyo ilifanyika tarehe 25 Septemba, 2021 iliambatana na kumbukumbu ya Somo wa Shule zetu Mwenyeheri Francis Maria Paul Libermann na pamoja na maadhimisho ya wiki ya Viziwi Duniani.
Waziri alionesha kufurahishwa na hatua ya uongozi wa shule hiyo kwa kuona umuhimu wa kusaidia watoto wenye mahitaji maalum na kuendesha harambee hiyo ili kuwa na vifaa na kuboresha masuala yanayowahusu ili kuwa na mazingira rafiki ya ufundishaji na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.
“Nimefurahishwa sana na uamuzi wenu wa kuadhimisha wiki hii ya Viziwi Duniani kwa kufanya harambee ya kupata fedha za uendeshaji na ununuzi wa vifaa maalumu vya kielimu na saidizi kwa wanafunzi wetu Wenye Ulemavu. Hongereni sana,”alesema Waziri Mhagama.
Waziri alieleza kuwa kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kwa mwaka 2019/2020, Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 55.9 ambapo milioni 2.5 kati yao ni Watu wenye Ulemavu. Aidha, kwa kipindi kirefu Watu Wenye Ulemavu wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali katika kutafuta fursa na huduma za kijamii ikiwemo elimu.
“Watu wenye ulemavu wamekuwa wakiachwa nyuma katika masuala mbalimbali likiwemo hili la elimu, niendelee kuiasa jamii kuwapa kipaumbele na kuwawezesha ili wapate elimu itakayotoa fursa ya kuonesha uwezo walio nao bila kujali hali zao,”alisisitiza Waziri Mhagama.
Akisoma taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu Bi.Edister Massawe alisema shule inalenga kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuto elimu bora kwa watoto wa Tanzania hasa wenye mahitaji maalum kama vile viziwi pamoja na kuwapa fursa watoto wenye ulemavu kupata elimu bora, kusaidia familia zao kwa kuwapatia ufadhili na udhamini kwa watoto hao ili wajikwamue kielimu.
“Shule hii ya Viziwi inatoa elimu hiyo bure na imejikita kuwasaidia ili kuwafanya wabadilike wawe wenye kujitambua, kugundua na kuendeleza vipaji vyao na kuwajengea uwezo kwenye nyanja za ufundi na biashara ili waweze kushiriki katika masuala ya ujasiriamali, utunzaji wa mazingira na afya,”alisema Edister.
Akiongoza ibada maalumu ya kuombea shule na kumbukumbu ya Somo wa Shule zetu Mwenyeheri Francis Maria Paul Libermann Padre Philip Athanas Massawe C.S.Sp, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu (Spiritans) Kanda ya Tanzania, alisema jamii iwe mstari wa mbele bila uoga kuwainua watu wenye mahitaji maalum kwa kuwajengea ujasiri na kuwatambua kwani kufanya hivyo ni sehemu ya ibada na kujipatia baraka mbele za Mungu kwa kuwaangalia wahitaji.
“Taifa tuondoe uwoga na kuwainua watu wenye ulemavu na kuwaona wanaweza na kuwainua bila kuacha kuwaombea kuyafikia malengo yao,”alieleza Padri Philip
AWALI
Shule ya Libermann Viziwi inamilikiwa na Shirika la Mapadri wa Roho mtakatifu (spiritans) Kanda ya Tanzania. Shule ipo kata ya Kawe, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.Shule ilisajiliwa rasmi tarehe 11 Septemba, 2019 na kupewa namba za usajili EM. 17973 yenye kaulimbiu isemayo “Moyo mmoja roho moja (One heart one Soul).Ni shule pekee ya viziwi inayotumia mtaala wa Kingereza kwa kufundishia na kujifunzia na ina uwezo wa kuchukua wanafunzia 210 kuanzia ngazi ya awali mpaka darasa la saba.
=MWISHO=