Habari
Waziri Lukuvi Awapongeza Maliasili kwa kutekeleza maono ya Mhe. Rais Samia
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutekeleza kikamilifu maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa Wizara ya kwanza kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi na kuwezesha Idara na Vitengo vyake kuhamia Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Waziri Likuvi ametoa pongezi hizo leo alipotembelea Wizara hiyo kwa lengo la kukagua ujenzi wa Majengo ya Serikali ambao ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu ya Serikali kuhamia Dodoma.
Mhe. Lukuvi amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii licha ya kukamilisha mapema ujenzi wa jengo hilo, inastahili pia kupongezwa kuwa wa kwanza kuhamia na kuwa mfano katika Matumizi ya samani za Ofisini zilizozalishwa hapa nchini kupitia mazao ya Misitu.
"Ninyi ni mabalozi wazuri wa Matumizi ya bidhaa zetu za hapa nchini zinazotokana na Misitu yetu, niimani yangu kuwa Wizara zote zitaiga mfano huu". Aliongeza Mhe. Lukuvi
Aidha Mhe. Lukuvi ametoa rai kwa watumishi wa Wizara hiyo kuhakikisha wanatunza vyema miundombinu na vifaa vilivyopo ili viweze kudumu kama ilivyo kusudiwa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amemshukuru Waziri Lukuvi kwa ziara yake, na kuahidi kuwa Wizara itatekeleza vyema maelekezo aliyoyatoa hususani ya usimamizi mzuri wa Matumizi ya jengo na vifaa vilivyopo.