Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Dkt. Chana “Wazee ni mabalozi wazuri wa Serikali kwa wananchi”


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi Pindi Chana ameomba Wazee wa Mji wa Dodoma kuendelea kuishauri Serikali katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Miradi ya Maendeleo zinazotekelezwa.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Baraza la Wazee wa Mji wa Dodoma na kupata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Mjini Dodoma hii leo (22 Januari, 2022).

Amesema kuwa Ujenzi huo unahitaji bajeti ya kutosha ili kukamilika kwa wakati huku akipongeza uongozi wa Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan umeonesha nia ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kimapinduzi kwa kuhakikisha kwamba Taasisi za serikali zinahamia Dodoma kwa wakati unaostahili.

Aliongezea kuwa, ujenzi wa miundombinu ya awali katika Mji wa Serikali  umekamilika,  huku  ujenzi wa Barabara za Mji wa Serikali Mtumba ukiwa  umekamilika kwa 94%. Kwa upande wa ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya Maji Safi, Maji Taka, Umeme Mawasiliano, Tehama, Usalama Zimamoto na Upandaji wa Miti ipo katika hatua za mwisho ya kuanza utekelezaji wake.

Alitumia nafasi hiyo kueleza mikakati dhabiti ya Serikali kuboresha Jiji la Dodoma huku akiwasihi wazee hao kuwa kinara na mabalozi wazuri wa Serikali yao kwa jamii.

 “Wazee ni Mabalozi wazuri wa serikali kwa wananchi, nyinyi ndiyo wadau wakubwa kwa kuhakikisha serikali inahamia Dodoma na Ujenzi wa miundombinu mingi umeendelea chini ya uongozi wenu, tuendelee kuunga mkono jitihada za serikali  zinazoongozwa chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Uchumi wa Nchi na kulinda Amani ya Nchi kwa maendeleo yetu,” Alisisitiza Balozi Dkt. Chana.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mjini Dodoma Mhe. Peter Mavunde amesema  wamefarijika kupata fursa ya kutembelea Mji wa Serikali Mtumba ambapo alieleza kuwa mji huo kuwa na historia ndefu toka ulipotangazwa na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere, na dhamira ya  kuhamisha Makao Makuu kuwa Dodoma ikaendelea kuwepo  katika Awamu zote za uongozi.

Ameeleza katika kuadhimisha miaka 60 ya uhuru, Serikali ya Awamu ya sita iliweka Mawe ya Msingi Katika wizara zetu ikiwa ni ishara ya kuwa makao ya kudumu katika Mji wa Serikali Mtumba na kueleza ilikuwa ni jambo la fahari kwa wazee wa Dodoma.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Dodoma  Mjini Meja Mstaafu Johnick Risasi amesema wazee wananafasi na jukumu la kuelimisha vijana ili wapate kuwa na urithi mzuri kwa Taifa lao na kujiletea maendeleo huku wakizienzi  amani, upendo na mshikamano

“Ili amani iwepo, kila mmoja wetu anapaswa kuitunza kwa sababu ni tunu muhimu na kwa wanaopewa madaraka katika nyadhifa mbalimbali lazima wawe na upendo, unyenyekevu, na kuheshimu watu,”alisema Risasi

 

=MWISHO=