Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Dkt. Chana akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani Nchini.


Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kuhakikisha hatua za uhifadhi wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi zinatekelezwa kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana Februari 11, 2022 Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Balozi Regina Hess ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi ikiwemo uhifadhi wa mzingira, kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Waziri Chana alisema uwepo wa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi husababisha wananchi kupata madhara na kuchochea uharibufu wa mazao hivyo ipo haja ya kuungana pamoja kama washirika ili kubadilishana uzoefu na kupata muafaka wa kudumu kwa changamoto hizo.

“Tumezungumzia masuala mengi upande wa Sera, Bunge ni namna gani tunaweza kushirikiana pande mbili na kuboresha mashirikiano yetu kati ya Tanzania na Ujerumani umoja huu utasaidia kulinda mazingira na kuboresha uharibifu wa mazingira usiwepo,” alisema Waziri Chana.

Pia Mhe. Chana alisisitiza kwamba Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka nje katika sekta mbalimbali na imeendelea kuboresha miundo mbinu itakayosaidia kuwekeza nchini kuchangia pato la Taifa na kutoa ajira kwa wananchi.

“Milango yetu kwa Diaspora na wawekezaji iko wazi tunawakaribisha sana wawekezaji waje kuwekeza katika sekta mbalimbali katika viwanda, uzalishaji, kilimo na nikuhakikishie kuwa tupo tayari kushirikiana na kufanya uratibu wa masuala ya uwekezaji ndani ya nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisisitiza Dkt. Chana

Aliongezea kuwa, Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania litaendelea kushirikiana na kulinda ushirikiano kati yake na Bunge la Ujerumani kwa maendeleo ya nchi zote mbili kudumisha uhusiano uliokuwepo tangu miaka ya nyuma.

Aidha Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regina Hess alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji na hivyo kuwavutia kuwekeza kwa wingi.

“Kipekee nampongeza Mhe. Rais kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji nchini hii imewezesha kuzitumia fursa zilizopo na kuendelea kuwekeza zaidi Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya,”alisema Balozi Hess.

=MWISHO=