Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Watu wenye Ulemavu wakopeshwa Tsh. Bilioni 12 kote Nchini: Naibu Waziri Ummy Nderiananga


SERIKALI imekopesha watu wenye ulemavu kiasi cha shilingi bilioni 12.9 hadi kufikia Agosti mwaka huu fedha zitokanazo na asilimia 10 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri kote nchini.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga wakati wa maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe Kitaifa ambayo yalifanyika Kibaha, Mkoani pwani. 

Naibu Waziri alieleza kuwa Watu wenye Ulemavu wana uwezo mkubwa wa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na za kiuchumi, hivyo kutokana na uwezo walionao wamekuwa wakiwezeshwa mikopo na halmashauri kupitia asilimia 10 yaani 4% kwa Vijana, 4% kwa Wanawake na 2% kwa Watu wenye Ulemavu.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini inayoonguzwa na MheshimiwaSamia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuratibu na kuweka sawa mipango ya kisheria, kanuni na taratibu za Watu wenye Ulemavu katika kutetea haki zao na kutoa huduma za msingi," alisema Naibu Waziri Nderiananga

Aidha, Naibu Waziri Ummy Nderiananga alitumia fursa hiyo kuwasihi Watu wenye Ulemavu kuhakikisha wanajitokeza kushiriki katika zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 2022, ili kupata kujua idadi yao kamili.

Aliongeza kuwa, kutokana na umuhimu wa Sensa ni vyema wenye Ulemavu kupitia vyama vyao wakawa mstari wa mbele kujitokeza kuhesabiwa ili kuisaidia Serikali katika kutambua idadi sahihi ya Watu wenye Ulemavu waliopo nchini na kuwafikishia huduma wanazohitaji kwa ukaribu.

“Ndugu zangu tunapoadhimisha Leo siku ya Fimbo Nyeupe ni lazima pia tukumbuke suala la Sensa lililopo mbele yetu na mimi Waziri wenu nachukua fursa hii kuwaomba wenzangu twende tukahamasishane kushiriki Sensa hiyo kwa faida yetu na faida ya Taifa letu,” alisema 

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ummy amewakumbusha Watu wenye Ulemavu nchini kuhakikisha wanajitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe na familia zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Sara Msafiri alisema kuwa mkoa huo umeendela kushirikiana na Watu wenye Ulemavu katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo hususani katika kuweka misingi yao imara itakayoimarisha ustawi wao.