Habari
Watanzania wahimizwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushiriki katika maonesho ya nane nane na kuleta baadhi ya Idara na Taasisi zake katika maonenosho hayo.
Ametoa wito huo Agosti 7, 2023 alipotembelea na kuzungumza na watumishi wa Ofisi yake walioshiriki katika maonesho ya Kimataifa ya kilimo maarufu Nane nane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Jiji la Mbeya na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu kuhusu mapambano ya virusi vya UKIMWI, masuala ya Menenjimenti ya Maafa, kujua shughuli zinazotekelezwa na Idara ya MpigaChapa Mkuu wa Serikali, shughuli za Baraza la Taifa la biashara pamoja na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II).
Amesisitiza wananchi waendelee kufika banda hilo ili kujifunza zaidi kujua namna ambavyo wanaweza kukabiliana kabla na baada ya majanga kutokea na kupata uelewa namna ambavyo Serikali inaratibu utekelezaji wa shughuli zake.
Akiongelea kuhusu kuhusu Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ameeleza kuwa ipo katika hatua ya kufanya tathmini ya kipindi cha miaka mitano na kueleza umma kwamba ipo haja ya kujifunza namna wizara zingine za kisekta yaani kilimo na uvuvi zilivyopiga hatua kuhakikisha sekta hizi zinaendelea kuleta tija kwa jamii.
"Kwa maana hiyo mimi niwakaribishe Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu tuendelee kushirikiana, tuendelee kujifunza kazi zinazofanywa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuzingatia jukumu lake kuu la kuratibu shughuli zote za Serikali,'' amesema Mhe. Ummy Nderinanga.
=MWISHO=