Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wananchi wa Bukombe wapewa somo kuhusu elimu


 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe  mkoani Geita, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu kwa kuwa ndio nguzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Amesema hayo Juni 7, 2024 wakati akihutubia mkutano wa wananchi katika Shule ya Msingi Bufanka iliyopo Kijiji cha Bufanka, Kata ya Bugelenga, Jimbo la Bukombe.

Serikali imeendelea kujenga shule ambapo kwa sasa Wilaya ya Bukombe ina shule za sekondari 7 na shule 5 za kidato cha tano na sita ambapo awali kulikuwa na shule moja.

“Naona aibu kuona watoto wanazuiwa wasiende shule, niwaombe wazazi tupeleke watoto shule. Wenyeviti wa Vijiji niwaombe kama kuna mtoto kwenye kijiji chako ambaye anatakiwa kwenda shule na haendi, nenda kwenye kaya hiyo kuwaeleza kuhusu umuhimu wa elimu ili mtoto huyo aweze kwenda shule”, amesisitiza Dkt. Biteko.

Vilevile, Dkt. Biteko amechangia ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa ya shule iliyopo katika Kata ya Bugelenga kwa kutoa mabati 135 na mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Dkt. Doto Biteko amewata wananchi wa Kijiji cha Bufanka na Jimbo la Bukombe kwa ujumla kujiandaa kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu kwa kuchagua watu wenye sifa watakaosaidia kuleta maendeleo.

“Viongozi wa Chama chetu na Katibu Kata anzeni kwenda kwenye kata zetu kuwaambia  mabalozi tukutane ili tujadiliane kuhusu uchaguzi, watu wengine wanashangaa Chama Cha Mapinduzi kinashindaje wajue tu ni kwa kuwa tunajipanga mapema kwa ajili ya kesho”, amesema Dkt. Biteko.

“Tujue watu wangapi wanapiga kura na nani anataka kugombea lakini niwaambie tu tusikubali kutumia rushwa, tuvipinge vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi. Viongozi wa kata na shina andaeni viongozi vizuri wenye sifa za kuchaguliwa ambao watasaidia kuleta maendeleo tunataka wilaya yetu iwe mahali salama pa kuishi kwa kuchagua watu wenye maono au mawazo mazuri yatakayosaidia utatuzi wa changamoto sio kuchagua mtu ilimradi tu ana fedha”, amefafanua na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.

“Napenda kuwajulisha kuwa Mhe. Rais atafanya ziara mkoani Geita na hapa Bukombe miradi mingi itakuja haya mnayoyaona tu ni sehemu. Na mimi kama mbunge wenu nina kazi ya kuhakikisha maendeleo ya kweli yanakuja katika maeneo yetu.”

Naye, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Festo Dugange amesema kuwa Dkt. Biteko amesemea miradi mingi  kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na Mhe. Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na zahanati.

“Hapo awali huduma zilikuwa mbali na gharama za kwenda kupata matibabu zilikuwa juu kakini Mhe. Dkt. Biteko aliona changamoto hiyo na alipomueleza Mhe. Rais Samia Wilaya hii ilipewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo”, amesema Mhe. Dugange.

Ameongeza kuwa Jimbo hilo pia limepata zaidi ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya sekta ya afya na Kata ya Bugelenga peke yake wamepata shilingi milioni 50 na maeneo mengine tayari wamepata fedha na zahanati zimejengwa. Pia, Mhe. Rais ameelekeza shilingi milioni 500 nyingine kwa ajili ya Hospitali  ya Wilaya ya Bukombe ambapo itajengwa  hospitali ya watoto njiti.

Akizungumzia daraja lililopo mpakani kati ya Bugelenga na Mbogo, Mhe.  Dugange amesema “ Serikali tayari imetenga shilingi milioni 585 kwa ajili ya ujenzi wa daraja, na shilingi milioni 85 zimeshaletwa hapa, TARURA wataanza kutafuta mkandarasi na katika kipindi cha ndani ya mwezi mmoja na nusu ujenzi wa daraja hili utaanza na baadaye tutaanza ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 30.”

Kuhusu sekta ya elimu, amesema kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne Jimbo hilo limepata zaidi  ya shilingi bilioni 9 kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari. Aidha, amewapongeza  wananchi kwa kuwa na mbunge hodari, mchapakazi na mwenye kujali na kutatua changamoto zao.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Bw. Nicholaus Kasendamila amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wa Bukombe kwa kuhakikisha wanapata maendeleo kwa kuwa na miradi mbalimbali  ikiwemo ya shule, hospitali na barabara.

Aidha, amewasihi wananchi wa Bukombe kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa “Huu  ni mwaka wa uchaguzi  tunatakiwa kujiandaa  na viongozi wa CCM katika Mkoa huo tuhamasishe wapiga kura kushiriki katika uchaguzi na hatimaye kuchagua viongozi  wazuri”.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rose Busiga amesema kuwa Mbunge wa Jimbo hilo Dkt. Doto Biteko ameendelea kutatua changamoto zao mbalimbali ikiwemo ya mawasiliano na tayari fedha za kujenga minara 9 ya mawasiliano zimeshaletwa jimboni.

Aidha, pamoja na mkutano huo wa hadhara wananchi wamepata fursa ya kuchangia damu, kupima afya pamoja na kupata elimu ya masuala ya lishe.

 

=MWISHO=