Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wanafunzi milioni 1.2 kujiunga na kidato cha kwanza mwakani


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wanafunzi 1,206,995 kati ya 1,397,370 waliohitimu darasa la saba mwaka huu wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari, mwakani.

“Wanafunzi 1,206,995 sawa na asilimia 86.4 ya wanafunzi 1,397,370 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2023 wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari Januari, 2024,” amesema.

Hayo yamesemwa leo (Ijumaa, Novemba 10, 2023) na Waziri Mkuu wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30, mwakani.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kukamilisha maandalizi muhimu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2024 ikiwemo ujenzi wa miundombinu. “Nitumie fursa hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote nchini wahakikishe kuwa ujenzi wa miundombinu yote katika shule za sekondari unakamilika kabla ya tarehe 30 Novemba, 2023.

Amesema Serikali itawachukulia hatua wote watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika shule za sekondari. “Wakuu wa Mikoa fanyeni ufuatiliaji, Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi katika Halmashauri zote nchini hivyo hakuna sababu wala visingizio vya kutokamilisha ujenzi kwa wakati,” amesisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kuandikisha watoto wa elimu ya awali 1,877,484 wenye rika lengwa wakiwemo wavulana 934,560 na wasichana 942,924 na darasa la kwanza 1,729,180 wakiwemo wavulana 860,870 na wasichana 868,310 ifikapo Januari, 2024.

“Hadi sasa jumla ya watoto wa elimu ya awali 407,138 sawa na asilimia 21.7 wakiwemo wavulana 201,244 na wasichana 206,253 wameandikishwa. Kati ya watoto wa elimu ya awali, wenye mahitaji maalum walioandikishwa ni 960 kati yao wavulana ni 488 na wasichana ni 472.

Amesema walioandikishwa kujiunga darasa la kwanza ni 593,452 sawa na asilimia 34.3 wakiwemo wavulana 293,728 na wasichana 299,724. Kati ya wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa wenye mahitaji maalum ni 1,365 wakiwemo wavulana ni 733 na wasichana 632,” amesema.

Amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini wasimamie zoezi la uandikishaji katika maeneo yao jambo ambalo amesema itakuwa vema likihitimishwa Desemba 31, mwaka huu“Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha wazazi na walezi wote wenye watoto wenye rika lengwa, wawaandikishe watoto hao ili waweze kuanza masomo ifikapo Januari, 2024.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kutokana na jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa pembejeo zikiwemo mbolea, hadi Oktoba 31, mwaka huu wakulima zaidi ya milioni 3.6 walikuwa wamesajiliwa na kupata namba za utambulisho za kununua mbolea ya ruzuku.

“Nitumie fursa hii kuwaelekeza Wakuu wa Wilaya ambao pia ni Wenyeviti wa Kamati za Pembejeo za Wilaya wawahamasishe wakulima kujisajili na kutoa taarifa sahihi kuhusu mazao wanayolima na ukubwa wa mashamba yao kwenye madaftari ya wakulima ambayo yamesambazwa kwa watendaji wa vijiji na mitaa ili taarifa zao ziweze kuingizwa kwenye mfumo na wapatiwe namba za kununulia mbolea ya ruzuku.”

Ameitaka Wizara ya Kilimo ihakikishe mbolea inapatikana kwa wakati na ishirikiane na Wakuu wa Wilaya kusimamia kwa karibu usambazaji wa mbolea kwa wakulima. “Hatua hii iende sambamba na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa usambazaji wa pembejeo hiyo muhimu,” amesisitiza.

Amezitaka kampuni na taasisi zinazozalisha mbegu bora ziongeze kiwango cha uzalishaji na kuweka utaratibu mahsusi wa kufikisha mbegu hizo kwa wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.