Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wadau wahimizwa kuunga mkono serikali kutokomeza vitendo vya ukatili


Wadau waaswa kuunga mkono jitihada za Serikali kutokomeza vitendo vyote vya ukatili, kwa kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunawezesha kutekelezwa mikakati yenye lengo la kutokomeza Ukatili dhidi ya makundi yote ikiwemo Wazee, Wanawake na Watoto.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa katika Maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Dodoma yenye kauli mbiu, “Ustahimilivu na mchango wa Wazee ni muhimu kwa Maendeleo ya Taifa”.

“Mabaraza ya Wazee kote nchini yashiriki kikamilifu katika juhudi za kutokomeza mauaji, kurithisha mila, maadili mema na uzalendo kwa jamii, na kuhamasisha vijana na jamii nzima kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji mali na ulinzi wa nchi yetu,” alisema Waziri.

Aidha Wananchi wote kwa ujumla kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kutoa taarifa na kuwafichua wahalifu ili kundi hili linalo tia doa nchi yetu liweze kudhibitiwa na pale tunapoona viashiria vya uhalifu na kutoa taarifa mapema kabla tatizo halijatokea.

Waziri amehimiza Madirisha ya wazee katika hospitali, vituo vya afya na zahanati yaimarishwe na kuhakikisha huduma kwa wazee zinatolewa kwa ukamilifu. Nielekeze Wakala wa Dawa za Serikali (MSD) kuhakikisha wanazingatia mahitaji muhimu ya wazee zikiwemo fimbo na viti vya kusaidia kutembea (wheel chairs) pindi wanapoagiza vifaa tiba au madawa na kuvisambaza katika maeneo ya kutolea huduma za afya.

Naye Mwenyekiti wa baraza la wazee Lameck Sando ameomba serikali kuongeza nafasi maalumu za kukaa wazee kwenye vyombo vya usafiri hasa Mijini na kwenye Majijiji.

“Kushirikisha mabaraza ya wazee ngazi zote katika zoezi la taifa la kuhamasisha chanjo ya UVIKO-19 na mengine yanayohitaji ushiriki wa wazee”.