Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wabunge waridhishwa na hatua za uwezeshaji vijana


Kamati ya Kudumu ya Bunge  ya Katiba na Sheria Yaridhishwa na  hatua iliyofikiwa katika kuwawezesha vijana takribani 3440 kukuza ujuzi wao kupitia programu  ya Ukuzaji ujuzi inayotekelezwa  na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,  Ajira na Wenye Ulemavu .

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Nagma Giga amesema kuwa mradi huo ni muhimu katika kuiwezesha nguvu kazi ya Taifa hasa vijana kuwa na ujuzi stahiki.

 “Tunaipongeza Serikali kwa mkakati huu utakaowezesha kupanua wigo wa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika nchi yetu”alisema Giga.

Mradi wa mafunzo ya ufundi stadi kwa Vijana unatekelezwa kupitia chuo cha ufundi stadi DONBOSCO kwa ufadhili wa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020 vijana elfu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo.

Akizungumza wakati wa ziara ya Wabunge hao mwishoni mwa wiki Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi,Vijana na Ajira Mhe. Antony Mavunde amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa nguvu kazi ya Taifa inakuwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya ujenzi wa uchumi wa Viwanda.

Aliongeza kuwa kuwajengea uwezo Vijana kwa kuwapa ujuzi stahiki kunawawezesha kujiajiri na kuzalisha ajira hali inayowawezesha kuchangia katika kukuza uchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu  Mhe. Stella Ikupa amesema kuwa Vijana wanayo nafasi kubwa ya kuchangia katika kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia ujuzi wanaopata kupitia programu hiyo.

"Pamoja na changamoto ya ajira kwa vijana, Serikali yetu sikivu imeendelea kuwapa kipaumbele vijana katika kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la ukosefu wa ajira kupitia utekelezaji wa programu hii itawezesha vijana wengi kujiajiri na kuchangia kukuza uchumi"

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Msaki amesema kuwa uwezeshaji Vijana umepewa kipaumbele kupitia programu hiyo na utaratibu huo ni endelevu kwa dhamira yakuwafanya vijana wachangie katika kukuza uzalishaji na tija.

Wakizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo Katika Chuo cha Ufundi Stadi DONBOSCO cha Jijini Dodoma baadhi ya wanufaika akiwemo Bi.  Esther Ngallya amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuwawezesha Vijana kujikwamua kiuchumi kupitia programu ya kukuza ujuzi inayotekelezwa kupitia chuo hicho.

Akiafafanua amesema kuwa Serikali imebadili mwelekeo wa maisha ya Vijana walionufaika na Programu hiyo ambao wanauwezo mkubwa kwa sasa nyanja za umeme, ujenzi, tarazo,useremala, umeme, ufundi bomba na nyingine nyingi.

Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwawezesha Vijana kupitia programu mbalimbali ikiwemo ya kukuza ujuzi na ile ya ujenzi wa vitalu nyumba katika kila Halmashauri ambapo vijana 100 katika kila halmashauri wanajengewa uwezo ili waweze kutekeleza azma ya kuchangia katika kukuza uchumi na ujenzi wa viwanda.

=MWISHO=