Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Utitiri wa kodi watesa wafanyabiashara Morogoro


Wafanyabishara wa Mkoa wa Morogoro wamelalamikia utitiri wa kodi ambazo wamedai ziko zaidi ya 15 na kuiomba serikali kuwa na kapu moja la kodi badala ya kila taasisi kuwa na kodi yake na kumwendea mfanyabishara kwa nyakati tofauti huku wazabuni wakilalamikia kutokulipwa fedha zao.

Malalamiko hayo yamewasilishwa na mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoani Morogoro Ally Mamba mbele ya mawaziri na manaibu waziri 10 katika mkutano wa mashauriano kati ya serikali,wafanyabiashara na wawekezaji ambapo mbali na malalamiko ya kodi wamedai kuwa hakuna meza ya majadiliano kati yao na halmashauri ili kuangalia namna ya kuboresha shughuli zao.

"waheshimiwa mawaziri changamoto ya taasisi moja moja kutoza kodi ni kikwazo kikubwa kwetu na ni kero wakati umefika sasa serikali iangalie namna ya kuboresha mfumo wa utozaji kodi ili tuweze kufurahia kulipa kodi badala ya kuona kero"alisema Mamba

Kwa upande wa mwakilishi wa wazabuni amedai kuwa muda mrefu hawajalipwa na serikali hadi baadhi yao wamepoteza maisha na wengine wamefilisiwa.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakiwemo wafugaji wameeleza changamoto ya soko la maziwa inayowakabili na kuiomba serikali kuwatafutia wawekezaji watakaojenga viwanda vya maziwa mkoani humo.

Aidha wamesema maeneo ya malisho ni madogo kwani tangu watengewe wafugaji wameongezeka na kuomba maeneo ambayo yamefutwa na serikali wapewe wafugaji ili kupunguza migogoro na watumiaji wengine wa ardhi.

Pia wameomba kwenye minada ya mifugo kuwepo na mizani ya kupima kabla ya kuuza ili mkulima aweze kunufaika na ufugaji na kuongeza kuwa kuwepo na kituo maalum cha kuuza ngozi kwani kwa sasa wengi wanazitupa.

Wakijibu malalamiko hayo na mengine kuyatatua papo hapo mawaziri hao akiwemo naibu waziri wa fedha Ashantu Kijaji amesema Mkoa wa Morogoro TRA wanalalamikiwa na wanaongoza kukusanya kodi kwa nguvu na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.

Akijibu malalamiko ya wazabuni amesema wote wamelipwa ambao bado watakuwa walikuwa wapigaji na kama yupo mwenye vielelezo apeleke kama viko sahihi atalipwana kwamba serikali imeshalipa zaidi ya shilingi milioni mia mbili kwa wazabuni wote wanaopeleka vyakula mashuleni.

Kwa upande wake Naibu waziri ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira mh Mussa Sima amepiga marufuku NEMC kumrudisha mwekezaji akabadilishe matumizi ya ardhi.

" kama ikionekana haifai kwa ajili ya anachotaka kuwekeza serikali na taasisi zake wawasiliane suala la kuwaangaisha wawekezaji halikubaliki kuanzia sasa wawekezaji kaeni mkao wa kula" alisema Sima

Akihitimisha mkutano huo Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Angella Kairuki amesema serikali itaendelea kuboresha baadhi ya sheria na hivi karibuni zitapelekwa bungeni kwa ajili ya marekebisho lengo ni kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki

Wawekezaji wawe tayari kutoa maoni juu ya sheria ya uwekezaji kwani iliyopo hivi sasa ni ya muda mrefu na imepitwa na wakati.

"ni kweli tozo nyingi zimefutwa lakini niendelee kuwaomba mawaziri kuziangalia ambazo bado ni kikwazo na kero kwa wananchi ziendelee kufanyiwa maboresho"alisema Kairuki

MWISHO