Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

“Ujenzi wa nyumba za waathirika wa maafa Hanang’ uzingatie ubora na thamani ya fedha,” Waziri Mhagama


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama amehimiza ujenzi wa nyumba za waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope, miti na mawe Wilayani Hanang’ Mkoa wa Manyara uzingatie viwango na thamani ya fedha ili kuhakikisha hatua ya kurejesha hali kwa wananchi hao inakuwa yenye viwango na ubora unaotakiwa.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari tarehe 10 Februari, 2024 mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua na kujionea maendeleo ya hatua za kurejesha hali katika maeneo mbalimbali Wilayani humo yalipotokea maafa hayo Disemba 3, 2023 na kusababisha vifo, uharibifu wa mali pamoja na miundombinu ikiwemo barabara.

Waziri Mhagama amesema, Serikali imeona umuhimu wa kujenga nyumba 108 zitakazotumika na waathirika wa maafa hayo ambapo eneo lililotengwa ni Gidagamowd lililopo katika Kitongoji cha Waret ambalo lina ukubwa wa Hekari 100 na tayari viwanja 269 vimepimwa.

“Mhe Rais wetu amejali sana, na ameonesha moyo kama mama kuamua kutenga eneo hili maalum na kutoa maelekezo ya kuhakikisha wale wote waliopata changamoto hii wanapata makazi mapya, hivyo ni muhimu kutimiza maagizo haya kwa viwango vya juu na ubora unaotakiwa,” alieleza

Aidha amesema kuwa, ujenzi huo uende sambamba na ujenzi wa shule, vituo vya afya na kituo cha polisi ili wananchi wapate huduma za kijamii kwa wakati na urahisi wawapo hapo.

Amezitaka Taasisi zote zinazopaswa kuhakikisha huduma muhimu zinaanza kupatikana ikiwemo; umeme, maji na barabara zikamilike kwa wakati bila kukwamisha zoezi la ujenzi wa nyumba hizo.

“Ni lazima taasisi zetu ikiwemo TANESCO na TARURA mjitahidi kurahisisha upatikanaji wa huduma zenu hasa ya kuchonga barabara hii ili kuwe na urahisi wa mawasiliano na kuhakikisha wakandarasi hawakwami na kazi ya ujenzi inaanza mwezi huu wa Februari na tunataraji ukamilike mapema Mei, 2024,” alisisitiza Waziri Mhagama

Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau walioendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika hao huku akiwaomba wengine kuendelea kufanya hivyo ili hatua hiyo ya kurejesha hali ikamilike na wananchi warejee na maisha yao kama awali.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Janeth Mayanja amemshukuru Mheshimiwa Waziri Mhagama kwa kuendelea kuratibu kila hatua ya masuala ya menejimenti ya maafa huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha adhma ya kukamilisha ujenzi huo inafikiwa.

“Tutaendelea kuwahudumia ndugu zetu kwa hatua zote, hadi sasa zoezi la ugawaji wa vifaa vya misaada vinaendelea vizuri na kwa utaratibu uliopangwa, hili la kusimamia ujenzi wa makazi ya ndugu zetu tutalifanya na kuhakikisha linakamilika kwa ushirikiano wa pamoja,” alieleza Janeth

 

=MWISHO=