Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Tuimarisheni ufanisi katika utendaji kazi – Dkt. Yonazi


KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kuimarisha ufanisi katika utendaji kazi wa kila siku ili kufanikiwa katika kufikia malengo ya Serikali.

Ameyasema hayo mapema leo Machi 9, 2023 katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi na aliyekuwa katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. John Jingu, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum.

“Endelezeni ushirikiano katika maeneo yenu ya kazi na naamini kuwa, kila mtumisi ni kiongozi katika eneo lake, na hili linaweza kuleta tija katika utendaji na kuwaletea Faraja watanzania tunaowahudumia katika nchi yetu.” Alisistiza Dkt. Yonazi

Dkt. Yonazi aliendelea kuwaasa wafanyakazi hao, kufanya kazi kwa ushirikiano, upendo na amani ili kuleta matokea chanya.

“Naamini tutaendelea kushirikiana namimi na mnipe mawazo yenu katika utendaji wetu, tuweke juhudi zetu, kwani tuna kazi ambayo Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ametupa nafasi na tuitumie kwa ushindi.”alisisitiza.

Kwa hatua nyingine akizungumza na wajumbe wa menejimenti ya ofisi hiyo mara baada ya makabidhiano rasmi ya ofisi aliwaasa kuwa vielelelezo na kuwaongoza wengine kwa upendo, umoja, amani huku wakitumia nafasi zao katika kujali kila mtumishi katika nafasi yake pasipo kuwabagua.

“Niwaombe viongozi wote, tuchukie kuongoza watumishi wasio na furaha, wapeni watu nafasi na kuwaheshimu kwa kuelewa tabai zao na kuchukuliana mapungufu tukiamini kuwa umoja ni nguvu utengano ni dhaifu,”alisema Dkt. Yonazi.

Awali, akiongea katika makabidhiano hayo aliyekuwa katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. John Jingu, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara  ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, aliwashukuru Menejimenti na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu kwa  kushirikiana naye vizuri kwa kipindi chote alichotumikia Serikali katika Ofisi hiyo na kuwaomba kuendelea na moyo huo wa ushirikiano.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa TUGHE katika Ofisi Hiyo Bi. Numpe Mwambenja akitoa shukrani kwa niaba ya Watumishi wa Ofisi hiyo alimshukuru Katibu Mkuu Dkt Jingu kwa kuwajengea ujasiri na kuondoa uwoga katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

=MWISHO=