Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Tanzania kuwa mwenyeji Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi Wanachama kutoka Kusini na Mashariki mwa Afrika.


Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi Wanachama kutoka Kusini na Mashariki mwa Afrika utakaofanyika Jijini Arusha kuanzia Oktoba 23 hadi 27 mwaka 2023.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akiongoza kikao cha maandalizi ya mkutano huo kilichohudhuriwa na Makatibu Wakuu ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala muhimu yatakayojadiliwa.

Dkt. Yonazi amesema mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan akisema Nchi  wanachama wa jukwaa hilo ni pamoja na  Kenya, Uganda, Namibia, Zimbabwe, Eswatini, Msumbiji, Seychelles, Botswana.

Nchi nyingine ni Angola, Zanzibar, Malawi, Lesotho, Mauritius, Zambia na Afrika ya Kusini ambapo mkutano huo utafanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Jukumu la Mahakama za Nchi Wanachama katika Utatuzi wa Migogoro chini ya Utangamano wa eneo Huru la Biashara la Afrika: Matumizi ya Teknolojia ya Kisasa kwa Ufanisi katika Utoaji Haki”

=MWISHO=