Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali yasisitiza matumizi ya mfumo wa pd-mis mkoani Arusha


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu imehimiza watendaji wa Halmashauri zote za Jiji la Arusha matumizi ya Mfumo wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu.

Hayo yamesemwa katika Mafunzo yavitendo yaliyofanyika katika kata nne za jiji hilo ikiwa ni muendelezo na hitimisho la mafunzo ya mfumo wa PD-MIS yaliyowakutanisha wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na maafisa ustawi wa jamii na TEHAMA jutoka Halmshauri zote za jiji la Arusha, yaliyochukua siku tatu ambapo makundi ya watu mbalimbali ya watu wenye ulemavu yamejitokeza kuitikia wito wa kujisajili katika mfumo.

Akizungumza wakati wa kilele cha mafunzo hayo, Afisa kutoka kitengo cha huduma kwa watu wenye ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Gerold Komba ametoa shukrani za dhati Uongozi wa Mkoa na Maafisa ustawi wa jamii na Maafisa TEHAMA kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo tangu siku ya kwanza, Aidha aliwapongeza baadhi ya watu wenye ulemavu waliojitokeza kushiriki .

Amesisitiza kuwa ujuzi uliopatikana utakuwa nguzo muhimu katika kutekeleza majukumu ya msingi ya ukusanyaji wa na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu.

Mafunzo haya yanatazamwa kama hatua ya kimkakati ya kuhakikisha Maafisa na Watendaji  wanakuwa na uelewa mpana wa kutekeleza majukumu yao katika kuwahudumia watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kukusanya na kusimamia taarifa za watu wenye ulemavu mkoani humo,jambo litakalosaidia kuimarisha  upatikanaji wa takwimu sahihi na kuimarisha na kuobresha upatikanji wa huduma kwa watu wenye ulemavu na kuinua Uchumi kwa watu wa Kundi hili.