Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali yaelekezwa kuongeza nguvu mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeshauri serikali kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI katika maeneo ya migodi; vituo vya magari makubwa, maeneo ya mialo ya samaki na maeneo ya starehe kwa kuangalia namna ya bora kutoa elimu kwa wananchi ili kujenga uelewa wa pamoja.

 

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masula ya UKIMWI Mhe. Mhe. Stanslaus Nyongo katika Ukumbi wa Mikutano wa Bunge Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia randama ya Bajeti ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania –TACAIDS kwa Mwaka wa fedha 2024/2025.

 

Ameongeza kusema upo umuhimu wa kuweka vituo vya kisasa vya kusambazia mipira (kondomu) ambazo mhitaji anaweza kuweka tokeni na kupata, utaratibu ambao ni  mzuri kabisa na utaondoa utaratibu wa kuchukua mipira hiyo kiholela.

 

“Kuna baadhi ya sehemu wameanza kutumia mfumo huo wa kisasa wa kusambaza mipira, nasi tuna nafasi ya kuhimiza  kuwekwa kwa vifaa hivyo maeneo mbalimbali ya uwekezaji na maofisini  kwa sababu tumepitisha Bajeti hii ili muweze kufanya Kazi vizuri ,” alibainisha.

 

Tunahitaji malengo mliyoyakusudia yatekelezwe na yanatimizwe vizuri ili wananchi wapate mazingira mazuri ya kuishi na kuondokana na hali ya maambukizi ya UKIMWI ambayo yanafanya watu waishi katika hali ya wasiwasi.

 

Aidha niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI na nimpongeze Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mafanikio tuliyoyapata kwenye yale malengo ya 95, 95, 95.

 

“Utafiti umeonesha kwamba kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI kinazidi kupungua na tunakazi kuendelea kusimamia sekta nyingine kuhakikisha mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI yanafanikiwa, “Alifafanua.

 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu ) Mhe. Jenista Mhagama alisema serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kupima hususani kwa wanaume kwa kuwa wamekuwa wakijitokeza kwa idadi ndogo.

 

“Tunahitaji kurudisha tena ile kampeni ya FURAHA YANGU iliyoongozwa na Mhe.  Waziri Mkuu, kuanza tena kwa mwaka ujao wa fedha angalau tuhamasishe kiwango kikubwa cha wanaume wajitokeze kupima VVU,” alifafanua

 

Serikali kwa kushirikiana na Baraza la watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI; Viongozi wa dini na Vongozi wa kijamii tutaendelea kutoa elimu ya kupinga unyanyapaa na ubaguzi kupitia majukwaa yao, makongamano na vipindi vya redio.

 

Awali Mhe. Dkt. Christina Mnzava aliomba serikali kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kuongeza mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI ili kufikia lile lengo la kufikia 95 ya Mwisho.

 

Naye Mhe. Cecil Mwambe aliomba serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wakinababa WAVIU kuwa na uwezo wa kushiriki na kujihusisha katika vikundi kwenye shughuli za miradi ya maendeleo.