Habari
Serikali kuendelea kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kukabiliana na maafa.
SERIKALI itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kukabiliana na maafa ambayo husababisha madhara makubwa kwa wananchi ikiwemo uharibifu wa miundombinu pindi yanapotokea.
Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya wakati akifungua kikao kazi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuthibitisha Mpango wa Dharula wa Kukabiliana na Maafa kilichofanyika Januari 26, 2022 Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Mmuya alisema mpango huo umeainisha shughuli zitakazofanywa na sekta mbalimbali kwa ajili ya kuzitekeleza kuweka mbinu bora za kuzuia madhara yatokanayo na ukame kupitia rasilimali zilizopo nchini kupata matokeo chanya huku akieleza kuwa katika mpango wa dharula ambao Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu kupitia Idara ya Menejimeti ya Maafa hadi kufikia hatua ya kupata rasimu yake ni jukumu la wote kuboresha na kuthibitisha ili uanze kutumika.
“Maafa ni kitu ambacho kinakuja bila kutegemea hivyo serikali inajitahidi sana kutoa ushirikiano kutoka kwa mashirika na wadau mbalimbali kutatua ama kutoa huduma mbalimbali katika maeneo yaliyo kumbwa na majanga. Pia serikali inatambua mchango wenu mashirika ya kimataifa (WFP) ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Emergence Coordination Group na pia Agricaltural Working Group ambao ni wadau muhimu Sana na wadau wengine wa maendeleo,” alisema Mmuya.
Aidha alitoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushirikiana na Serikali ya Awamu hii katika nyanja mbalimbali zinazolenga kuleta maendeleo ya Taifa na kuendelea kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabili majanga katika maeneo husika ili shughuli za kiuchumi na kijamiii kufanyika katika mazingira rafiki na salama.
Sambamba na hilo aliwaasa wananchi kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kupata elimu na kufahamu tahadhari za kuchukua endapo kutatokea mabadiliko ya hali ya hewa ama mabadiliko ya tabia nchi.
“Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania kwenye utabiri wake wa Septemba 2021 na mwezi Novemba hadi Aprili umeonesha mvua za msimu zitakuwa chache kwa baadhi ya maeneo nchini hali itakayosababisha ukame, kukauka kwa mabwawa, malambo ya maji na kupungua kwa malisho ya mifugo”,alieleza
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa wa Ofisi hiyo Kanali Matamwe Said alieleza kwamba mkutano huo umefanyika kwa lengo la kufanya maandalizi ya kujiandaa na athari zinazoweza kutokea kutokana na utabiri ulio tolewa na Mamlaka ya Hali Hewa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye jukumu la kuratibu shughuli za serikali kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imeamua kukutana na wadau kujadili Mpango huo endelevu ili kuanza kutumika bila kuchelewa kama tunavyofahamu maafa huwa hayatoi taarifa yanatokea wakati ambao hujayatarjia hivyo, serikali haiwezi kukaa kimya lazima ichukue hatua kukabili ili wananchi wake wafanye shughuli zao kwa utulivu,” alibainisha Mkurugenzi huyo.
=MWISHO=