Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya Watu Wenye Ulemavu


SERIKALI imesema inaendelea na utaratibu wa kujenga na kukarabati vyuo vya watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwasaidia wenye ulemavu kupata ujuzi ili kujikomboa kiuchumi.

Akizungumza  Jijini Dodoma baada ya kupokea msaada  wa vifaa visaidizi kwa ajili ya  wenye ulemavu vyenye thamani ya shilingi milioni 13.9  ambavyo ni  viti mwendo  55 na fimbo nyeupe 50 za wasioona  kutoka kwa  Taasisi ya  kutoa huduma ndogo za kifedha (ASA Microfinance Company Limited), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alisema dhamira ya Serikali ni  kuhakikisha kila mtanzania anapata haki yake bila vikwazo.

Aliongeza kuwa ipo mikakati madhubuti ya kuhakikisha masuala ya wenye ulemavu yanapewa kipaumbele ikiwemo uboreshwaji wa vyuo  ikiwemo Chuo cha Mwanza ambacho ujenzi wake unatarajiwa kukamilika kuanzia mwezi Januari mwakani  kuwawezesha vijana   kupata mafunzo ambayo yatawasaidia kufanya shughuli zao za uzalishaji na kushiriki katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

"Kwasasa Wizara inaratibu kwa kasi ujenzi wa vyuo vya watu wenye ulemavu na ufufuaji wa vile ambavyo vipo.Tunaendelea kufanya hivyo katika Chuo cha Yombo Dar es salam,  tumezindua Chuo kingine Tabora ambacho kilikuwa kimefungwa kwa miaka 10 na kumalizia ujenzi wa  chuo cha kisasa Mkoa wa Tanga," alisema Naibu Waziri Ummy.

Pia Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo kuwasaidia watu wenye ulemavu  kwa kuendelea kutoa fedha ya elimu bila malipo ambapo  watu wenye ulemavu nao hunufaika na mfumo huo huku akieleza kuwa Serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.

"Serikali kupitia bohari kuu ya dawa inaendelea kuagiza mafuta ili kuwakinga dhidi ya saratani ya Ngozi kwa watu wenye ualbino  sambamba na kuzitaka Halmashauri kuendelea kutenga fedha za mapato ya ndani kupitia asilimia 10 inayotolewa na kila Halmashauri kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu  kwa sababu hii inawasaidia kupambana na umasikini,"alieleza.

Hata hivyo aliishukuru kampuni hiyo kwa moyo wake wa kujitoa na kuiunga mkono serikali katika juhudi za kuwaletea ustawi wananchi wake na kuwahimiza wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuwasaidia watu wenye ulemavu hatua itakayofanya kujiona wana thamani na kutambulika ndani ya jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji  wa ASA Microfinance Limited , Muhammad  Shah Newaj alieleza kwamba  wametoa  msaada huo wenye thamani ya Sh. milion 13.9  kama sehemu ya kutambua mchango wa watu wenye ulemavu katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa akisema wana uwezo wa kufanya  kazi kama watu wengine endapo watapewa fursa na kuhudumiwa katika mahitaji yao wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanaisaidia jamii kuepukana na umaskini.

Naye Afisa Sheria kutoka ASA Microfinance Limited, Zephania Paul alifafanua kwamba  vifaa hivyo ni sehemu ya kutoa huduma kwa jamii na awamu hiii ni yapili kufanyika akisema awamu ya kwanza ilifanyika jijini Dar es salaam huku akibainisha kuwa  taasisi hiyo ipo katika Mikoa nane ya Tanzania Bara na Zanzibar  na hadi sasa wamewafikia  wanawake 1,600 na kutoa ajira .

 Akitoa shukrani zake mama wa mtoto mwenye ulemavu  Martha Mshama aliishukuru serikali kwa kushirikiana na wadau kuendelea kuwajali watu wenye ulemavu  akieleza kuwa kiti alichopewa  kitamsaidia  kufanya kazi zake kwani  awali alikuwa akitumia muda mwingi kuwa karibu na mtoto akihofia kuanguka na kupata madhara.

" Tunaishukuru serikali kwa kutupatia viti mwendo ambapo ni msaada mkubwa kwangu maana nilikuwa nikihofia usalama wa mtoto wangu kuna wakati anaweza kuanguka natakiwa kuwa naye karibu sana lakini sasa walau nitaweza kufanya kazi zangu nawashukuru sana Mungu awabariki,”alishukuru Martha.

Naye Selina Nigangwa (mwenye ulemavu wa miguu) mkazi wa Swaswa aliishukuru serikali kwa kuwapatia msaada huo kwa kuzingatia walikuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kabla ya kuwa na vifaa hivyo na kuamini msaada huo utaleta tija katika maisha yao ya kila siku.

=MWISHO=