Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali Imepiga Hatua Kubwa katika Kudhibiti VVU na UKIMWI Nchini – Waziri Mhagama


Serikali imepiga hatua katika kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa mujibu wa upimaji wa hiari wa Maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) umeongezeka nchini kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi asilimia 83 mwaka 2019.

Hayo yamebainishwa leo November 14,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na Waandishi wa Habari  kuelekea maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Desemba 1, 2021.

Waziri Mhagama amesema kuwa kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilima 61 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2019.

”Kufuatia watu kuwa na mwamko wa upimaji huo umechangia kupunguza pia kiwango cha maambukizi mapya katika jamii kutoka asilimia 7 mwaka 2003/2004 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/2017”amesema Waziri Mhagama

Amesema katika kuelekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru nchi imepiga hatua kubwa pia katika kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa wastani wa asilimia 50 kutoka watu 64000 mwaka 2010 hadi watu 32000 mwaka 2020.

Aidha amesema kwa upande wa kiwango cha kufubaza VVU kwa wanaotumia waathirika wanaotumia ARV kimeongezeka kutoka asilimia 87 mwaka 2016 hadi asilimia 92 mwaka 2019 huku matumizi ya dawa hizo kwa waathirika pia yakiongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi 98 mwaka 2019.

“Kufuatia mafanikio hayo tunajitahidi kuzuia maambukizi mapya ya VVU na tumefanikiwa kupunguza maambukizi hayo kwa watu wazima kwa miaka 15 na zaidi kutoka watu 110,000 mwaka 2010 hadi 68000 mwaka 2020

Waziri Mhagama amesema kuwa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka huu 2021 yanatarajiwa kufanyika kitaifa Jijini Mbeya kuanzia Novemba 24 hadi Disemba 1, 2021 katika Uwanja wa Luanda Nzovwe ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo Waziri Mhagama amesema kuwa licha ya kuwepo na mafanikio katika mapambano dhidi ya UKIMWI  bado kuna maeneo ambayo yanahitajika nguvu zaidi ili kutokomeza VVU na UKIMWI  ifikapo Mwaka 2030 kama inavyoelekezwa katika malengo ya Kidunia.

Waziri Mhagama ameyataja baadhi ya  maeneo ambayo yanatakiwa kuwekewa mkazo zaidi kuwa ni pamoja na kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI na VVU  hasa kwa Vijana kwani zaidi ya theluthi  moja ya Maambukizi mapya hutokea kwa Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 hususani Vijana wa kike.

Amesema ikiwa Vijana wataelekezwa namna ya kujikinga na maambukizi mapya na kukubali kujikinga,hali ya usambazaji virusi hivyo itapungua na itakuwa nafuu kwa Vijana wengine.

“Nawasisitiza vijana ukimwi bado upo,lazima kila mmoja akubali kumkinga mwingine hii itatusaidia kuokoa nguvu kazi ya taifa na kuipa unafuu Serikali katika kugharamia masuala ya ukimwi,”amesema.

Mhagama amesema kuwa katika  wiki ya maadhimisho hayo kutakuwa na matembezi ya hisani kwa ajili ya kutangaza na kuhamasisha uchangiaji wa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund – ATF) ambayo yatafanyika tarehe 24 Novemba, 2021 Mbeya. 

”Kutakuwa na Kongamano ambalo litahusisha mawasilisho ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI nchini. Pia kutakuwa na mdahalo wa vijana wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati vilivyopo Mkoani Mbeya ambapo watajadiliana masuala mbalimbali yanayo husiana na afua za VVU na UKIMWI kwa vijana, mafanikio yaliyofikiwa vyuoni katika kukabiliana na changamoto hizo pia kutakuwa na Mdahalo wa Viongozi wa Dini na Viongozi wa Jadi (Machifu), utakaohudhuriwa na vijana na jamii kwa ujumla”amesema

Hivyo ametumia fursa kuwahimiza Wakazi wa mkoa wa Mbeya na mikoa jirani watumie fursa ya maonesha hayo kupata elimu ya afya,ushauri nasaha,upimaji wa hiari wa VVU , Upimaji wa Saratani ya Shingo ya Kizazi, Sukari, Uwiano wa Urefu na Uzito wa Mwili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko ameishukuru Serikali kwa kuendelea kupambana na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Naye Mwenyekiti wa Baaza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bi Leticia Kapela ameishukuru Serikali kwa kuwajali wanaoishi na virusi vya Ukimwi hususan katika kuleta chanjo ya Uviko 19 ambayo ni muhimu zaidi kwao.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutujali sisi watu tunaoishi na virusi vya UKIMWI na sisi Baraza tutahakikisha tunashirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI,” amesema Bi Letia 

kauli mbiu ya maadhimisho ya Mwaka huu 2021 ni “Zingatia Usawa. Tokomeza UKIMWI. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko