Habari
Ruangwa yatoa mikopo ya vifaa vya sh. milioni 357 kwa wajasiriamali
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 357 kwa vikundi vitano vya wajasiriamali vilivyotolewa kwa mkopo na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Waziri Mkuu amekabidhi vifaa hivyo leo (Jumamosi, Februari 27, 2021) katika viwanja vya shule ya msingi Likangara, wilayani Ruangwa na kuwataka wanufaika wa mikopo hiyo wakaitumie kama ilivyokusudiwa na wahakikishe wanarejesha kwa wakati.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kuamua kutoa mikopo ya vifaa mbalimbali kwa wajasiriamali na pia ameitaka ihakikishe inawasimamia vizuri wanufaika hao.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Frank Chonya alisema halmashauri yao imeendelea kutenga na kutoa mikopo kwa vikundi vya ujasiriamali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani.
Mkurugenzi huyo alisema kwa mwaka 2020/2021, Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imetoa mikopo mikubwa yenye thamani ya sh. milioni 357 ambazo wanavikundi wamenunua vifaa kwa ajili ya shughuli zao na wengine wameanzisha biashara ndogondogo.
Amesema halmashauri ilifanya utafiti na kuunda vikundi vitano vya kimkakati ambavyo vimepewa mikopo yenye thamani ya sh. 319,910,000. “Vikundi viwili vyenye wanufaika 20 ambavyo vinajishughulisha na ufugaji wa kuku, vimepewa mkopo wa shilingi 13,010,000 na wamenunua kuku 2,000 aina ya chotara.”
“Kikundi kingine ni cha vijana 39 wanaofyatua matofali ambacho tumekipa mkopo wa shilingi milioni 186, ambapo wameweza kununua lori la tani nane la kusombea mchanga na kubebea tofali, mtambo wa kufyatulia tofali, mifuko ya saruji 600 na fedha zingine ni kwa ajili ya shughuli za uendeshaji.”
Amesema kuwa kikundi kingine kilichonufaika na mkopo huo ni Jukwaa la Wanawake Ruangwa lenye wanufaika 37 ambalo linajishughulisha na usafi wa mazingira lililopewa mkopo wa sh. milioni 72.5 ambazo wamezitumia kununulia trekta na tela lake na vifaa vya kufanyia usafi. Kikundi hicho kinafanya usafi kwenye mji wa Ruangwa.
Mkurugenzi huyo amesema kikundi kingine kilichonufaika na mkopo huo ni cha vijana 10 wanaojishughulisha na uendeshaji wa bodaboda na bajaji ambao wamepewa mkopo wa sh. milioni 48.4 na wameweza kununua bajaji tano na pikipiki nne.
Baada ya kupokea vifaa hivyo, wanufaika hao waliishukuru Serikali kupitia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ruangwa kwa kuamua kuwakopesha vifaa kwa kuwa vitawezesha kuboresha shughuli zao za ujasiriamali na kwamba watahakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili wananchi wengine waweze kunufaika.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepokea msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10 kutoka kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola Kwanza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola Kwanza, Bw. Salum Nassor amesema kampuni yao imekabidhi madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10.
Nassor amesema wametoa msaada huo ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha elimu nchini, hivyo wamewaomba wadau wengine wa maendeleo wajitokeze na kushirikiana na Serikali kuhakikisha shule zinakuwa na madawati ya kutosha.
-Ends-