Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Rais Magufuli atunukiwa tuzo na Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly


UONGOZI wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, kupitia Kamati Kuu na Halmashauri Kuu umemtunukia tuzo ya uongozi Rais Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wake, ambapo Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani.

 

Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo (Jumapili, Desemba 20, 2020) kwenye ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, Dkt. Yohana Masinga iliyofanyika katika makao makuu ya kanisa hilo, Area C Wajenzi, jijini Dodoma.

 

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na Rais mwenye hofu ya Mungu na katika hotuba na maelekezo yake kwa viongozi na watendaji wa Serikali, amekuwa akisisitiza suala la kumtanguliza Mungu wanapowahudumia wananchi. 

 

“Ama kwa hakika hofu ya Mungu aliyonayo kiongozi wetu ndiyo hasa siri ya kufanikiwa kwa uongozi wake na Taifa letu kwa ujumla. Sote ni mashuhuda kwamba Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa nchi ya mfano Afrika na dunia kwa ujumla katika kupiga vita rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma sambamba na kurejesha nidhamu ya kazi ambayo ilikuwa imepotea katika ofisi za umma.”

 

Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha hivi karibuni, dunia nzima imeshuhudia jinsi Tanzania ilivyomtanguliza Mungu wakati wa mlipuko wa Homa Kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID19). “Tanzania hatukujifungia ndani kama mataifa mengine. Tuliendelea na shughuli zetu kwa imani kabisa tukijua yupo Mungu ambaye ndiye kinga na msaada wetu pekee.”

 

“Binafsi sitachoka kutambua na kutoa pongezi maalumu kwa viongozi wa dini nchini kwa namna walivyoshirikiana na waumini wao katika kuiunga mkono Serikali kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 na katika kipindi chote hicho mmekuwa mkiwapatia Watanzania faraja sambamba na kuwatia moyo wagonjwa kwamba Mwenyezi Mungu atawaponya. Hatua hizo zimekuwa mhimili mkubwa wa upendo, umoja, mshikamano na ujasiri miongoni mwa Watanzania. Tunawashukuru sana.”

 

Ametumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kujenga mustakabali wa sasa na wa baadaye wa nchi yetu. Kadhalika, Serikali inathamini mchango wa madhehebu ya dini katika kutoa huduma za jamii hususan elimu, afya, maji na makundi maalum yenye uhitaji wakiwemo yatima, wajane na wengineo.

 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa viongozi wote wa dini nchini watambue umuhimu wa majukumu yao kiroho, kuthamini wito walionao na dhamana ya kuwaongoza watu katika maeneo yao ya ibada na jamii yote inayowazunguka kwa uaminifu na unyenyekevu mkubwa kama ilivyoelekezwa katika vitabu vya dini.

 

“Viongozi wetu wa kiroho napenda mtambue kwamba ninyi ni vioo kwetu. Kwa msingi huo, tukiwa wafuasi wenu nasi tunapaswa kujiona kupitia ninyi. Serikali inatambua na kuthamini kazi na majukumu makubwa ya viongozi wa kanisa ambayo ni pamoja na kutoa mafundisho ya kiroho, kuwaongoza watu kiroho na kimwili, kuwasaidia katika shida zao za kiroho, kutoa ushauri katika mambo yahusuyo mafundisho na maisha ya kiroho na kuwajenga watu kiimani.”

                                                                                                        

Amesema kusimikwa kwa Askofu Dkt. Masinga kunadhihirisha kazi nzuri na njema ambayo amekuwa akiifanya katika kumtumikia Bwana na ni ishara ya imani kubwa kutoka kwa waumini wote wa kanisa hilo na pia walio nje ya kanisa hilo. “Leo unapokabidhiwa nafasi hii, tunayo imani kubwa kuwa utalitumikia kanisa kwa moyo na kudumisha utulivu miongoni mwa waamini wote na Watanzania kwa ujumla.”

 

Waziri Mkuu amesema jukumu alilokabidhiwa leo la kuwa Askofu Mkuu wa Makanisa ya Philadelphia Afrika, Asia na sasa Marekani siyo jukumu dogo ni kazi inahitaji hekima kuu ili kuwaongoza watu hao wa mataifa hayo yote kiroho na kimwili. Amempongeza kwa maono hayo makubwa ya kuanzisha kanisa ambalo hadi sasa linapotimiza miaka 30, limeweza kuenea ndani na nje ya Tanzania.

 

“Sote tumezoea kuwaona Wamisionari kutoka nje wakija kuhubiri na kutuletea madhehebu mbalimbali, lakini wewe umefanya tofauti. Kanisa hili limeanzia Tanzania na umekuwa mmishonari wa kulipeleka nje ya Tanzania. Sote kwa pamoja tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ampe hekima na nguvu ya kuliongoza kanisa.”

 

Waziri Mkuu amesema hivi sasa maeneo mengi nchini yameingia kwenye msimu wa kilimo na sehemu mbalimbali zimeanza kupata mvua, hivyo ametoa rai kwa Watanzania wote kuongeza bidii kwenye kilimo ili waweze kupata mavuno mengi yatakayolihakikishia Taifa usalama wa chakula na kuwapatia ziada ya kuuza ndani na nje ya nchi. “Kwa kufanya juhudi na bidii katika kazi tutakuwa tukitekeleza maelekezo ya maandiko matakatifu pamoja na maagizo ya Serikali yetu.”

 

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagiza mamlaka zinazohusika mipango miji zitenge maeneo ya ibada. “Natambua kuwa ipo miongozo kuhusu hili ambayo husimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Hata hivyo, naelekeza kuwa mamlaka zinazohusika na mipango miji kuendelea kutenga maeneo kwa ajili ya ibada kuanzia vijijini.

 

“Tengeni maeneo rasmi ya ibada! Serikali yetu haina dini lakini wananchi wake wana dini. Kutotenga maeneo ya ibada ni kuwanyima wananchi haki na uhuru wa kuabudu. Hivyo, ninasisitiza kwa Halmashauri zote zizingatie utaratibu kuwa michoro yote ya mipango miji haina budi kuonesha maeneo ya ibada na yamilikishwe kwa madhehebu husika bila kubadili matumizi ya maeneo hayo.”

 

Kwa upande wake, Askofu Masinga amesema kanisa limetoa tuzo ya utumishi uliotukuka kwa Rais Dkt. Magufuli baada ya kutambua kazi njema na bora ambayo imefanyika chini ya uongozi wake uliojaa hekima, umakini, ujasiri bila ya kuyumbishwa na watu na hivyo kuliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kati kabla ya wakati uliotarajiwa.

 

“Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly na uongozi wake tumeona na kutambua kazi njema na bora ambayo imefanyika chini ya uongozi wako, ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za Taifa kama madini yetu, hifadhi za Taifa na kuwakumbuka wanyonge ukisisitiza wapewe haki zao. Tunakuombea baraka na afya njema wewe na familia yako,” amesema.

 

(mwisho)