Habari
Rais Dkt. Samia ni kiongozi imara, amedhamiria kuwahudumia watanzania-Majaliwa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi imara ambaye amedhamiria kuwahudumia Watanzania kwa kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia katika maeneo yao.
Amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipoweka mawe ya msingi ya Miradi ya Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi ya Ziwa Victoria kutoka Ziba hadi Nkinga na Makomero hadi Mgongoro, wilayani Igunga mkoani Tabora, Machi 12, 2025.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa Ziba hadi Nkinga unaogharimu shilingi bilioni 2.49 na kutarajia kuhudumia wananchi 32,979, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za maji safi na salama nchini ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi kwa asilimia 100.
“Ndugu zangu wananchi, mradi huu ni matokeo ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, kuweni na uhakika kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni kutekeleza majukumu yenu ipasavyo kwasababu tunaye kiongozi madhubuti”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kulinda mazingira na vyanzo vya maji ili vitumike ili viweze kutoa huduma endelevu ya maji. “Tunamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuongeza bajeti ili wizara ya maji imudu kupeleka maji hadi vijijini lengo ni wananchi wapate maji kwenye maeneo yote”.
Mradi wa maji Makomero hadi Mgongoro umegharimu shilingi milioni 840.8 na unatarajia kudumia wakazi takribani 5,400. Mradi huo umefikia asilimia 80 ya ujenzi na unahusisha ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji, ukarabati wa vituo sita vya kuchotea Maji, ukarabati wa manywesheo mawili ya mifugo, kuchimba mitaro ya kulaza bomba na kufukia mitaro mita 25,000.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kuhakikisha anatenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Mwamayoka, Igunga mkoani Tabora.
“Mkurugenzi hakikisha unaanza ujenzi wa zahanati katika eneo hili, sio sawa wakazi wa eneo hili kutembea umbali wa takribani kilomita 20 kufuata huduma”
Akizungumza wakati akikagua vibanda vya biashara vilivyojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Halmashauri hiyo kutafuta njia nzuri ambayo itawawezesha wafanyabiashara kunufaika na uwepo wa vibanda hivyo badala ya kutumia utaratibu wasasa.
"Ninawapongeza sana kwa uamuzi wa ujenzi wa vibanda hivi, ni jambo kubwa ambalo litawawezesha wafanyabiashara wetu kuwa na maeneo ya uhakika ya ufanyaji wa biashara, lakini angalieni huu mfumo wenu, oneni namna mtakavyoweza kutafuta utaratibu mzuri wa kuwapatia wafanyabiashara”
Kwa upande wake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Wizara hiyo itaendelea kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji inaendelea kuimarika ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Pia, Mheshimiwa Aweso amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanatenda haki na kuepuka kuwabambikiza wananchi bili za maji.“Mwananchi atakayechota maji alipie kulingana na kile alichokitumia”