Habari
Rais Dkt. Samia anatambua mchango wa bunge kwenye kuhamasisha michezo-Majaliwa
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Juni 21, 2025 amemuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika tamasha la Grand Bunge Bonanza lililofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.
Akizungumza katika bonanza hilo, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatambua na kuthamini mchango wa Bunge la Tanzania katika kuimarisha umoja, Afya na mshikamano kupitia michezo mbalimbali.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa tamasha hilo ni sehemu ya makakati wa bunge wa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia za kuhamasisha watanzania kushiriki mazoezi ya viungo na lina mchango mkubwa katika kuhamasisha uwepo wa utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili
“Mazoezi haya mliyoyafanya kupitia Grand Bunge Bonanza yana umuhimu mkubwa si tu kwa afya, bali pia yanajenga urafiki na uhusiano mwema miongoni mwetu lakini pia yanaimarisha afya ya akili na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa majukumu yetu ya kila siku kwenye maeneo yetu”
Kwa upande wake, Naibu Spika Mussa Azzan Zungu amempongeza Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson kwa kuasisi bonanza la bunge ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwaleta pamoja wabunge kushiriki michezo mbalimbali
Naye, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Festo Sanga amesema kuwa bonanza hilo ni matokeo ya Maamuzi ya Spika wa Bunge Dkt. Tulia ya kuamua kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamaisha michezo ili kuwa na Taifa imara na lenye Afya. “Asante sana Serikali kwa kuhamasisha wananchi kushiriki michezo”
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema michezo ni moja ya ajenda muhimu ya benki ya CRDB “Michezo si afya bali ni ajira na ni sehemu ya kuibua vipaji mbalimbali kwenye jamii, bonanza hili ni maalum, muhimu na lakipekee”