Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Prof: Ndalichako “Vijana jiungeni kwenye vikundi mpate mikopo”


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Mhe,Prof, Joyce Ndalichako amewataka vijana waliopata mafunzo ya ukuzaji ujuzi katika vyuo mbalimbali nchini kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika na fursa za mikopo na vifaa kwa kujiendeleza kiuchumi.

Ametoa wito huo hii leo (29 Januari, 2022) mkoani Kigoma  mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ambapo vijana wa programu hiyo wanapata mafunzo kwa vitendo na kusisitiza kuwa lengo la  serikali ni kuona elimu hiyo inawanufaisha vijana.

‘Mheshimiwa Rais tayari ametupatia fedha kwa ajili ya kununua vifaa ambavyo tutavigawa kwa baadhi yenu, na kwenye ofisi ya Waziri mkuu kuna mfuko kwa ajili ya kuwawezesha vijana hivyo jiungeni kwenye vikundi ili mnufaike na fursa hizo niwambie tu mama hawezi kuwaacha  vijana wake” ,alisema Waziri Ndalichako.

Aidha amesema progamu hiyo ni endelevu ambapo awamu ya kwanza imepangwa kugharimu shilingi za Kitanzania bilioni tisa kwa matarajio ya kuwanufaisha zaidi ya vijana 14,000 kote nchini.

“Kwa niaba ya vijana hawa nimshukuru sana Mhe. Rais kwa maono yake kwakweli  amelitengeneza jeshi kubwa ambalo naamini kwa ujuzii huu tutapunguza sana utegemezi,”Alisisitiza prof. Ndalichako

Aliongezea kuwa kundi la vijana ni muhimu katika jamii kwa kutambua mchango wake hivyo limepewa kipaumbele katika kuwajengea uwezo ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.

Alitumia fursa hivyo kuwaasa baadhi ya mafundi ambao wamepata ujuzi katika mfumo usiyo rasmi kutumia fursa ya kurasimisha ujuzi wao ili waweze kutambulika na kunufaika na fursa za kiuchumi zinazojitokeza nchini.

Baadhi ya vijana walionufaika na mafunzo hayo akiwemo Aman Ahamad Rutta anayesomea masomo ya ufundi bomba na Mariam Hussein Ramadhani anayesomea ufundi umeme  wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafunzo hayo  na kuomba kuendelea kuwafikia kwa wingi ili kuendelea kupunguza changamoto za ajira na kuwa na vijana wenye uwezo wa kujikimu na kujiletea maendeleo yao.

“Kwakweli Serikali imekuja kutufungua macho sisi ambao tulikuwa tumebaki kama kundi la mwisho mtaani maana  tumejifunza vizuri yaani naamini baada ya hapa mimi binafsi nitakuwa na sehemu nzuri ya kuanzia”,alisema Rutta.

Kwa uande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe, kanali Isack Mwakisu amewataka vijana hao kuzingatia mafunzo wanayoyapata ili yawasaidie kunufaika na fursa za  ajira kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali wilayani humo.

Naye Mkuu wa chuo cha FDC Kasulu Mhandisi Ramadhan Simba amesema katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo wamepokea vijana 257 katika fani mbalimbali ikiwemo; ufundi wa magari, uashi, uselemara na ushonaji.

AWALI

Katika ziara hiyo Waziri Prof,Joyce Ndalichako ametembelea vijana hao katika maeneo mbalimbali wanayopatiwa mafunzo kwa vitendo ikiwemo   Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kigoma, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kasulu.

Programu hiyo ya kukuza ujuzi inayoratibiwa  na Ofisi ya Waziri Mkuu  inatokana  na utafiti wa Nguvu Kazi ya Taifa wa mwaka 2014 uliobaini kuwa asilimia kubwa ya watanzania wana ujuzi kwa kiwango cha chini.

 

=MWISHO=