Habari
Ofisi ya Waziri Mkuu yakamilisha mafunzo ya uendeshaji call centre, kuimarisha huduma kwa wananchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM -SBUU) imefanikiwa kukamilisha mafunzo ya watumishi wake kuhusu uendeshaji wa Kituo cha Taifa cha Mawasiliano na Simu (National Call Centre -NCC), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha utoaji wa huduma bora za kisasa za kusikiliza na kutatua kero kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Dar es Salaam ambapo washiriki walipata ujuzi wa kina kuhusu usimamizi wa mawasiliano kwa wananchi, mbinu bora za kuhudumia wananchi pamoja na matumizi ya mifumo ya kisasa ya call centre.
Mtoa Mada Katika mafunzo hayo Bw. Willynevilline Msamo kutoka Benki ya NMB amesema watumishi hao wamejengewa uwezo wa kushughulikia mawasiliano kwa ufanisi zaidi, kuongeza kasi ya utoaji wa huduma, na kuhakikisha kila mwananchi anayewasiliana na taasisi anapata msaada unaostahili kwa wakati.
Aidha, Bw. Msamo emeongeza kuwa kupitia uanzishwaji na uimarishaji wa huduma za call centre, Ofisi ya Waziri Mkuu inalenga kutatua changamoto za wananchi kwa haraka kwa kuweka mfumo rahisi na wa moja kwa moja wa kupokea na kushughulikia maoni, malalamiko na mapendekezo yao. Huduma hii itawawezesha wananchi kupata mrejesho kwa wakati, kufuatilia masuala yao kwa ufanisi, pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za serikali. Mfumo huu unatarajiwa kuwa daraja muhimu kati ya wananchi na taasisi, ukihakikisha sauti za wananchi zinasikika na kupatiwa ufumbuzi stahiki kwa wakati.
Hatua hii inaonesha dhamira ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya kuendelea kuboresha mifumo ya mawasiliano na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa haraka, kwa ufanisi na kwa viwango vya juu zaidi.




