Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Nyaraka za Mpango wa Usimamizi wa Kukabiliana na Maafa Kinondoni wazinduliwa


MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Saad Mtambule amezindua na kukabidhi nyaraka za Mpango wa Usimamizi na Mpango Mkakati wa namna ambavyo Watakabiliana na Majanga na Maafa kwenye Wilaya ya Kinondoni.

Akizungumza mara baada ya kuzindua na kukabidhi nyaraka hizo Machi 31,2023 Jijini Dar es Salaam, Mhe.Mtambule amesema yale yaliyobainishwa kwenye nyaraka hizo ni majanga ya kweli, ni majanga ambayo tunaishi nayo na yamekuwa yakitokea mara kwa mara.

Amesema kuna wajibu wa kusoma nyaraka hizo kwa wale wote waliokabidhiwa na baadae kuchukua hatua za utekelezaji wa mipango ambayo wameiandaa kukabiliana na maafa na majanga mbalimbali katika Wilaya hiyo.

Pamoja na hayo amewataka wadau wa afya pamoja akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuhakikisha wanafuatiliana kuhamasisha usafi wa mazingira pamoja na kuhamasisha watu wakae kwenye maeneo bila kutiririsha maji machafu.

Kwa upande wake Mratibu wa Masuala ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi.Winfrida Ngowi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ilitekeleza mradi wa kuimarisha uwezo wa Wilaya katika kupunguza vihatarishi vya maafa na kujenga jamii stahimilivu dhidi ya majanga.

Amesema lengo la utekeleaji wa mradi huo ni pamoja na kuweka mgawanyo wa majukumu kwa wadau wote waliopo katika Wilaya pamoja na kuainisha rasilimali zilizopo na kuweka mikakati endelevu na ya muda mrefu ya kupunguza vihatarishi vya maafa ikiwa ni pamoja na kuandaa mikakati ya namna ya kuwajengea uwezo wananchi.

Aidha amesema katika utekelezaji wa mradi huo ilifanyika tathmini ya kubaini vihatarishi vya maafa, uwezekano wa kuathirika na uwezo wa jamii kuzuia, kujiandaa na kukabili maafa.

"Tathmini hii ilifanyika katika mitaa ambayo ni Mtaa wa msisiri A (Kata ya Mwananyamala), Mtaa wa Kigogo (Kata ya Kigogo) na Mtambani (Kata ya Mzimuni) na Mtaa wa Mkunduge (Kata ya Tandale). Vigezo vilivyotumika kuteua mitaa hiyo ni suala la kujirudia kwa maafa ya mafuriko katika mitaa hiyo". Amesema

Amesema tathmini ilifanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 6 -10 Machi, 2023 ambapo timu ya tathmini iliundwa na wataalam 14 ambapo wataalam watano (5) walitoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wataalam tisa (9) walitoka Idara na Vitengo vya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, na mtaalam mmoja alitoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.

Hata hivyo amesema tathmini ya vihatarishi vya maafa katika Wilaya ya Kinondoni ilibaini kuwa Majanga makuu yanayoikabili Wilaya ya Kinondoni ni mafuriko na magonjwa ya mlipuko. Majanga mengine yaliyotajwa ni ajali za barabarani na ajali za moto na vilevile baadhi ya miundombinu ya kutolea huduma muhimu kwa jamii kama vile elimu ipo katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko.

Vilevile amesema walibaini kuwa Wanawake, Watoto, watu wenye ulemavu na wazee huathirika zaidi na maafa ikilinganishwa na makundi mengine katika jamii pia Jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na mtu mmoja mmoja ili kupunguza vihatarishi vya maafa.

Nae Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi.Twiningile Mwakalukwa ametoa wito kwamba, Mpango na Mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa ulioandaliwa uwe chachu ya ushirikishaji jamii na wadau, kujenga uelewa kwa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji tahadhari ya awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara, na kujiandaa kukabiliana na maafa.

Amesema mkakati wa Kupunguza Vihatarishi vya Maafa katika Wilaya ya Kinondoni ni hatua nzuri kuelekea katika ujenzi wa jamii stahimilivu dhidi ya majanga katika hii ya Kinondoni.

Ameeleza kuwa mkakati huo ni kitendea kazi muhimu cha kusaidia katika kuingiza masuala ya usimamizi wa maafa katika mipango ya maendeleo ya Idara, Vitengo na Taasisi zilizopo katika Wilaya . Aidha, Mkakati huu ni dira katika kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa katika Wilaya ya Kinondoni.

 

=MWISHO=