Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Naibu Waziri Ummy apongeza zoezi la upandaji miti Mji wa Serikali Dodoma.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amepongeza zoezi la upandaji wa miti katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa pragramu ya upandaji wa miti iliyofanyika tarehe 01 Juni, 2022 iliyozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Mhe. Ummy alisema zoezi hilo litakuwa na manufaa kwa Jiji la Dodoma kwa kuzingatia kuwa ni makao makuu ya Nchi hivyo inapaswa kuwa na muonekano wa kuvutia utakaohamasisha ukuaji wa uchumi.

“Serikali imezindua wa programu ya upandaji miti zaidi ya 550,000 ya aina mbalimbali itakayopandwa katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Serikali kama hatua ya uhifadhi wa mazingira,” alisema

Akielezea kuhusu ujenzi wa mji wa serikali alibainisha kuwa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje (Outer Ring Road) yenye urefu wa kilomita 112.3 unaendelea vizuri ambayo pia itapunguza msongamano katika Jiji la Dodoma, Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato umeanza ambao utawezesha kuhudumia abiria zaidi ya milion 1.5 kwa mwaka na utaruhusu ndege kubwa ikiwamo za aina ya Airbus 380 yenye uwezo wa kubeba abiria takribani 500 kutua na kuruka katika uwanja huo.

“ Maandalizi yanaendelea ili kujenga, kuboresha na kukarabati barabara mbalimbali katika jiji letu ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko wa ndani pamoja na upanuzi wa barabara ya Dodoma Mjini hadi Chamwino kwa upana wa njia mbili mpango utakaokwenda sambamba na uboreshaji wa barabara ya kuanzia Dodoma hadi Morogoro ambapo Mshauri Elekezi yupo katika hatua za ubunifu wa barabara hiyo,”alisema Mhe. Ummy.

Aliongeza kwamba programu ya upandaji miti inayozinduliwa ni  sehemu ya uendelezaji wa Mji wa Serikali ambayo inakwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mingine ya huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo 24 ya Wizara yenye urefu wa kuanzia ghoroga 6 hadi 11 ambayo yanaendelea kujengwa katika Awamu hii ya Pili ambapo ujenzi wake kwa sasa umefikia wastani wa kati ya 28% -40%.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dk. John Jingu alisema tayari ujenzi umefanikiwa katika hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu  baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo 23 ya Ofisi za   Wizara zilizojengwa Awamu ya Kwanza, tayari Serikali imetoa Shilingi Bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu Dodoma.

“Fedha hizi pia zimewezesha kuanza kwa ujenzi wa majengo 24 ya ghorofa ya Ofisi za Wizara yanayoendelea kujengwa katika Awamu ya Pili ambapo ujenzi wake kwa sasa umefikia wastani wa 28% hadi 40%. Ujenzi wa majengo haya unatarajiwa kukamilika kabla mwezi Oktoba, 2022”, Alisema Dkt. Jingu.

Katibu Mkuu huyo aliongezea kwamba, hadi sasa miundombinu ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 51.2 unaotekelezwa na Kampuni ya CHICO chini ya usimamizi wa TARURA umefikia 99% na Taasisi za huduma za DUWASA, TANESCO, TTCL, TPDC, TEMESA, eGA na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zipo katika hatua za kukamilisha taratibu za manunuzi ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

“Utekelezaji wa programu hii utafanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na TARURA hususani katika maeneo ya barabara na utasimamiwa na Timu ya Watalaam wanaoratibu ujenzi wa Mji wa Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu”,Alisisitiza Dkt. Jingu.

Aidha, ili kuhakikisha programu hii inafanikiwa, Ofisi ya Waziri Mkuu itaingia Mikataba ya Makubaliano na Wizara pamoja na Taasisi zitakazotekeleza programu hii kwa lengo la kuhakikisha kwamba miti inapandwa na kutunzwa kikamilifu ili kukamilisha dhana ya kuwa na Mji wa Serikali wa kijani na wa kuvutia.

 

=MWISHO=