Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Naibu Waziri Nderiananga awataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia


Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga na Mbunge wa Viti maalum amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyompatia ya kumteua kuwa Naibu Waziri.

Ametoa shukrani hizo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro ambapo alipata fursa ya kuzugumza na wananchi katika kijiji cha Lotima ambapo ndipo alipozaliwa katika Kata ya Makuyuni Mkoani humo Julai 18, 2023.

Amesema kuwa Rais anafanya kazi usiku na mchana hivyo watanzania wanapaswa kumtia moyo na kumuunga mkono ili aweze kufikia dhamira ya kuwaletea maendeleo endelevu.

"Mhe Rais Dkt.Samia ana upendo mkubwa na wana Kilimanjaro na sisi wanamakuyuni tumeona upendo wake, tumeona kujali kwake na kuthamini kwake kwa kuendelea kutuletea maendeleo," Alisema Mhe. Nderiananga.

Aliongezea kuwa Serikali imedhamiria kuwaleta wananchi maendeleo kwa kuendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo hivyo ni vyema kuendelea kuunga mkono kwa vitendo.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wana Lotima kwa mchango wao mzuri katika safari yake ya maisha na kuahidi ataendelea kuwapa ushirikiano wa hali na mali kadiri inavyowezekana.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Vunjo Mhe. Dkt. Charles Kimei amepongeza jitihada za Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo utengenezaji wa barabara ya Himo-Makuyuni kwa kiwango cha lami ambayo inaendelea kujengwa.

Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utarahisisha huduma za kijamii ikiwemo usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kisare Makori ameungana na Naibu Waziri Nderiananga kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa miradi mingi ya maendeleo katika Wilaya ya Moshi.

"Tumeendelea kupokea fedha za maendeleo kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioisha wa 2022/23, tuliletewa fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikiwa ya ujenzi wa shule , maeneo ya biashara na ukarabati wa barabara na hii imetupa faraja kama Wilaya na tumeiona nia nzuri ya Mhe. Rais," alisisitiza Mhe. kisare

Aidha alituma jukwaa hilo kuwasihi wananchi kuendelea kudumisha amani, upendo na utulivu katika maeneo yao na kupinga vitendo vya unyanyasaji wa aina yoyote ile.

"Hatutakubali kuona wananchi wanaonewa na kunyanyaswa kwa namna yoyote, kila mamlaka ifanye kazi kwa weledi na haki ili kuendelea kushiriki shughuli za uzaliahaji kwa utulivu, kujiletea maendeleo yetu wenyewe," aliongezea.

Alimalizia kwa kutoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa maeneo husika kunapotokea changamoto yoyote ya kiusalama ktk maeneo yao na kuwahakikishia Ofisi yake ipo wazi na itaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu.

 

=MWISHO=